Dkt Shein Awataka Wazanzibari kudumisha Amani na Utulivu

Baadhi ya Viongozi na watendaji wa Ofisi zililizondani
ya Mkoa wa Kusini Pemba wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Viongozi
hao katika mkutano wa majumuisho ya ziara aliyoifanya katika Mkoa huo
,uliofanyika ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro Vitongoji Pemba.[Picha na
Ramadhan Othman,Ikulu.]

WAZANZIBARI wametakiwa kuendeleza na kuimarisha umoja miongoni mwao bila kujali tofauti za kiitikadi huku wakidumisha amani, utulivu, upendo na mshikamano kuijenga nchi yao.

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kisiwa Panza kilichoko Wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba.

“tuishi kwa amani, tuonyeshane upendo bila ya kujali tofauti zetu za kisiasa ili kuimarisha amani na utylivu nchini kwetu kwa faida yetu sote”alisema Dk Shein.

Rais amesema viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeonyesha mfano mzuri ushirikiano miongoni mwao ndio maana Zanzibar inapewa heshma kubwa miongoni mwa mataifa ya nje.

“sisi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa tunaonyesha mfano..hapa tulipo kama sijasema kuwa tuko kutoka vyama tofauti hamtaelewa kwa sababu tunashirikiana, tunafanya kazi pamoja na tunafungua miradi pamoja kwa umoja wetu na ushirikiano wetu” alisisitiza.

Aliwataka Wazanzibari kuendelea kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala bora kwa kuendesha siasa za kistarabu bila ya vitisho wala kutukanana ili visiwa vya Zanzibar viendelee kuwa visiwa vya amani na utulivu.

“tunaweza kufanya siasa za ushindani bila ya kutukanana wala kudharauliana ingawa katika hali ya ushindani tunaweza kusemana lakini kwa njia za kistarabu bila ya kuvunjiana heshima”aliwaeleza wananchi hao.

Katika hotuba yake hiyo kwa mamia ya wananchi wa Kisiwa hicho ambapo awali alizindua kazi ya kulaza mabomba baharani kwa mradi wa kuimarisha huduma za maji katika kisiwa hicho Dk. Shein aliwataka wazanzibari kulinda heshma wanayopewa na mataifa ya nje kwa kuwa mfano bora wa kutatua matatizo yao.

“tumeithibitishia dunia kuwa tunaweza kushughulikia matatizo yetu wenyewe na hivyo kutujengea heshma kwa wenzetu wa nje na hivi sasa wameamua kushirikiana nasi kwa hali na mali harakati zetu za kuijenga zanzibar” alibainisha.

Dk. Shein alisema ni jambo la kujivunia wazanzibari kuona hivi sasa mataifa mengi yanaziunga mkono harakati zetu za kuendeleza nchi yetu kutokana na mazingira ambayo tumeyatengeneza sisi.

“Washirika wetu wa maendeleo wanakuja kushirikiana nasi na kutusaidia kwa sababu ya utekelezaji wetu wa demokrasia na utawala bora. Wanatupa misaada na wakati mwingine wanatukopesha kwa sababu tunakopesheka”alibainisha Dk.Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwaeleza wananchi hao kuwa uamuzi wa kufanya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010 yalikuwa maamuzi muhimu ambayo yameweka msingi wa maelewano miongoni mwa wazanzibari.

Maelewano hayo yamesaidia kuweka utulivu mkubwa nchini na kuweza kuifanya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuweza kufanya vizuri na kuleta ufanisi mkubwa kimaendeleo na kuimarisha amani na utulivu ikilinganishwa na nchi nyengine ambazo serikali zake zinafuata mfumo huo katika bara la Afrika.

Dk. Shein alisema kuwa kutokana na mafanikio na juhudi hizo ipo haja kwa wananchi kuishi pamoja na kuimarisha mapenzi yao ili kuijenga nchi yao licha ya kuwa kila mmoja anafuata sera na itikadi za chama chake.

Mapema alipowasili kisiwani humo kwa boti akitokea mji wa Mkoani, Dk. Shein alizindua awamu ya pili ya mradi wa kuimarisha huduma za maji Kisiwa Panza na baadae kukagua ujenzi wa madarasa ya skuli ya Sekondari Kisiwa Panza ambayo inajengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na washirika wengine ambapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iliahidi kumaliza ujenzi huo.