Waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seif Rashid anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya viziwi duniani itakayofanyika Septemba 27, 2015 kwenye viwanja vya Bwawani mjini Kibaha mkoani Pwani.
Hayo yamesemwa na Afisa Jinsia na Maendeleo kutoka Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Bi. Lupi Mwaisaka Maswanya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Bi. Mwaisaka amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kujenga mwamko wa jamii kuhusu haki za viziwi hususani utambuzi rasmi wa lugha ya alama kama njia ya mawasiliano kwa viziwi na fursa ya watoto viziwi katika maendeleo yao kielimu, kukuza vipaji, ushiriki kamilifu na katika kutimiza ndoto zao.
Aliongeza kuwa ujumuishwaji wa haki za matumizi ya lugha na alama ya Tanzania kwa watoto viziwi ili waweze kunufaika na elimu pamoja na fursa nyingine za kijamii na kuwawezasha viziwi na wataalamu kujadili changamoto zinazowakabili viziwi kupitia vyombo vya habari na kutoa fursa kwa jamii kuona uwezo na vipaji vinavyoweza kutoa mchango kwa maendeleo ya jamii.
Mwaisaka aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa wa Pwani wameaanda matembezi ya amani na mshikamano ambayo yataanzia katika viwanja vya TAMCO Kibaha hadi katika viwanja vya Bwawani ambapo shughuli nzima ya maadhimisho itahitimishwa.
Viziwi kote duniani husherekea wiki ya viziwi kimataifa mwezi Septemba kila mwaka ambapo vyama na asasi mbalimbali za viziwi huandaa matukio mbalimbali, matembezi, mijadala, kampeni na mikutano kuzungumiza masuala ya haki za binadamu ili kutengeneza daraja la ushirikiano na Serikali na jamii kwa ujumla.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Kwa haki za lugha ya alama ya Tanzania, watoto wetu wanaweza’’ ikimaanisha na kutambua mchango wa viziwi katika maeneo mbalimbali duniani, haki za binadamu kwa viziwi na maandalizi ya jamii ya viziwi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha ya badae.