HOTUBA YA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA KUWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA, ENEO LA KIBADA, DAR ES SALAAM,
Mheshimiwa Goodluck ole Medeye, Naibu Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;
Mheshimiwa, Said Meck Sadick, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam;
Ndugu Kesogukewele Masudi Issa Msita, Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa;
Ndugu Nehemia Kyando Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Nyumba la Taifa;
Menejimenti na Watumishi wa NHC Mliopo Hapa;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana:
Namshukuru sana Mheshimiwa Prof. Anna Tibaijuka, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ndugu Kesogukewele Msita, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba na Ndugu Nehemia Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa NHC na uongozi wote wa Shirika kwa kunialika kuja kushiriki katika tukio hili la kihistoria la kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na Shirika hapa Kibada.
Nawapongeza Bodi na Menejimenti ya Shirika kwa kubuni wazo hili zuri na kulitekeleza. Mmefanya uamuzi wa busara wa kujenga nyumba hizi kwa ajili ya watu wenye kipato cha kawaida. Uamuzi huu wa kizalendo unatoa taswira nzuri ya Shirika kwa jamii na kujenga imani miongoni mwa watu kuwa Shirika hili ni lao na lipo kwa ajili yao. Shirika sasa linajali hata maslahi ya watu wenye kipato cha chini na cha kati. Hii ndiyo ilikuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba mara baada ya Uhuru. Hili mnalofanya leo ndilo hasa jukumu lenu la msingi. Hongereni sana na naomba muendelee kufanya kazi hii mliyoianza.
Ndugu Wananchi;
Wananchi kuwa na nyumba bora za kuishi ni moja ya malengo makuu ya Serikali tangu uhuru wa nchi yetu miaka 51 iliyopita mpaka sasa. Ni hivyo, kwa sababu kuwa na nyumba ni mahitaji ya msingi ya mwanadamu. Lakini pia Serikali ililazimika kusisitiza kuwa na nyumba bora kwa sababu wananchi wengi walikuwa wanaishi katika nyumba za makuti. Hivyo basi Shirika lilianzishwa kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kuondoka kwenye nyumba za makuti na kuwa na nyumba bora. Ndiyo siri ya kujengwa na kuwepo kwa nyumba nyingi za “neshnali” Magomeni, Kinondoni, Mwananyamala, Ilala, Temeke, Mburahati, Buguruni na Keko kwa hapa Dar es Salaam na kwingineko nchini.
Nyumba hizo nzuri na imara zilijengwa na kuuzwa kwa gharama nafuu na watu wengi wenye kipato cha kawaida waliweza kumudu kuzinunua. Mpaka leo nyumba hizo zipo, tena bado imara kabisa licha ya kuwa na umri unakaribia miaka 50.
Kwa bahati mbaya kasi ya Shirika ya kujenga nyumba mpya za namna hiyo ilipungua hasa kuanzia miaka ya themanini kutokana na uhusiano wa nchi yetu na Ujerumani kutetereka na uchumi wa nchi kupata misukosuko kuanzia miaka ya 1970. Na baada ya nyumba za Msajili kukabidhiwa NHC, Shirika likasahau ujenzi wa nyumba. Shirika likabaki na kazi ya kukusanya kodi ya pango kwenye nyumba ilizojenga na zile zilizokuwa za Msajili. Kadri muda ulivyokuwa unakwenda Shirika likasahau kabisa wajibu wake wa kujenga nyumba. Lakini, si hivyo tu, hata makusanyo ya kodi pia yakaanza kudorora na uwezo wa kujiendesha wa Shirika ukapungua sana.
Hali hiyo, imekuwa mtihani mkubwa kwa Serikali kuhusu haja ya kulirejesha Shirika katika hali nzuri. Baadae Shirika likazinduka na kuanza tena ujenzi wa nyumba, lakini nyumba zake ni ghali sana ambazo watu wa kipato cha kawaida hawazimudu. Kwa kweli Watanzania wengi walioajiriwa hawazimudu hata wale wa vyeo vya juu, kwa vile mishahara yao bado si mikubwa. Bahati mbaya pia hapakuwepo na utaratibu wa mikopo ya nyumba baada ya kufa kwa Tanzania Housing Bank (THB) na mpango wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa umma.
Ndugu wananchi;
Kufuatia hali hiyo Serikali ikaamua kuchukua hatua za makusudi kuboresha Shirika na kuhuisha Sera na Sheria zinazohusu uendelezaji wa sekta ya nyumba ili ziendane na hali halisi ya wakati huu. Miongoni mwa hatua hizo ni kupata Bodi mpya na Mkurugenzi mpya. Pia, kutungwa kwanza kwa Sheria ihusuyo mikopo ya nyumba ili watu waweze kupata mikopo ya kujenga au kununua nyumba. Pili ni kutungwa kwa Sheria ya kuwezesha watu kuuziwa nyumba mojawapo katika ghorofa lenye nyumba nyingi na kupewa hati ya kumiliki nyumba hiyo. Utekelezaji wake umeanza, unaendelea ingawaje sijaridhika sana na kasi ya utekelezaji wa Sheria hizi mbili.
Pamoja na hayo, ujenzi wa nyumba unaendelea kwa kasi kubwa kote nchini kama tunavyoona wote. Hata hivyo, nyumba hizo ni ghali, watu wenye vipato vya chini na wafanyakazi si rahisi kumudu. Wengine hushawishika kufanya mambo yasiyostahili.
Nimefurahishwa sana na uamuzi wa Shirika la Nyumba la Taifa kwa uamuzi wake wa kujenga nyumba za gharama nafuu. Mmerejea kwenye madhumuni ya awali ya kuwepo kwenu. Sasa Shirika la Nyumba linafanya yale ambayo ilitumwa kufanya tangu kuasisiwa kwake.
Nimesikia kilio chenu kuhusu kodi ya ongezeko la thamani; bei za viwanja n.k. Wahusika wataambiwa. Pia, angalieni uwezekano wa kuwakopesha wafanyakazi kwa masharti ya kudhaminiwa na waajiri wao kuwalipa moja kwa moja.
Nashauri NHC nayo iangalie uwezekano wa kushiriki katika kuanzisha benki ya nyyumba au kuwa na hisa katika benki zilizopo. Kukiwa na utaratibu wa mikopo hususan yenye riba nafuu, wateja wa kununua nyumba watakuwa wengi na Shirika litanufaika. Mtajenga nyumba za gharama nafuu na wanunuzi watakuwapo.
Nawapongeza sana viongozi na watumishi wa Shirika kwa kazi nzuri muifanyao. Shirika limebadilika na mafanikio yanaonekana. Mmedhihirisha kwa vitendo kuwa mashirika ya umma yanaweza kufanya mambo mazuri. Endeleeni na moyo huo tupate mafanikio zaidi. Kinachotakiwa ni uongozi mzuri.
Mheshimiwa Naibu Waziri;
Ili ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini uweze kuwa endelevu ni lazima Serikali iweke mazingira mazuri ya kisera na kisheria. Inatupasa tuangalie namna ya kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba: kwa upande wa vifaa vya ujenzi kuwa vya gharama nafuu, gharama za viwanja, riba za mikopo, na kodi mbalimbali. Wizara ishirikiane na Wizara ya Fedha na Benki Kuu na taasisi za fedha ili kuangalia uwezekano wa kupunguza riba anayotozwa mnunuzi aliyechukua mkopo benki. Riba ya asilimia 18 ni kubwa mno. Tafadhali kaeni na taasisi zinazohusika mjadiliane ili kufanikisha utekelezaji wa sera yetu ya kujenga nyumba za gharama nafuu. Ni lazima tuendelee na utaratibu huu bila vikwazo ili watu wengi wanufaike. Maisha bora kwa kila Mtanzania yanahusu pia watu kuwa na nyumba bora za kuishi.
Vilevile ningependa Wizara yako ihakikishe kuwa Halmashauri zote nchini zinaharakisha kasi ya upimaji wa viwanja na kuviwekea huduma husika na kuviuza kwa bei nafuu. Halmashauri zisigeuze bei za viwanja chanzo cha kutafuta mapato na kumaliza shida zake. Itakuwa vigumu kwa Shirika la Nyumba kujenga nyumba za gharama nafuu kama Halmashauri zetu zitaendelea kuliuzia ardhi Shirika kwa bei kubwa. Mbona Halmashauri za Geita, Mvomero, Makete, Kongwa na Mkinga zimeweza kulipatia Shirika ardhi bila gharama yoyote. Iweje nyingine zishindwe kufanya hivyo? Halmashauri ikiliuzia Shirika viwanja kwa bei kubwa, gharama za nyumba zinakuwa kubwa na kupoteza dhana nzima ya unafuu.
Aidha, Wizara inalo jukumu la kuhakikisha kuwa maeneo mapya yanayopimwa yanakuwa na huduma zote muhimu kama vile umeme, maji, barabara na mawasiliano ya simu. Huu ni utaratibu wa msingi ambao hautekelezwi ipasavyo. Naomba tuangalia namna ya kuurejea utaratibu huu kwani utapunguza kero zisizokuwa za lazima.
Pia naomba Shirika la Nyumba liandae mpango wa ujenzi wa nchi nzima na kisha kuwasilisha mpango huo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mapema iwezekanavyo. Hali hii itawezesha Wizara na taasisi zinazotoa huduma kuweka mipango yao kulingana na kazi zilizo mbele yao. Mimi nina imani kuwa Shirika la Nyumba likipewa ushirikiano mzuri, gharama ya nyumba inazojenga itapungua zaidi.
Ndugu wananchi;
Napenda kuwaahidi kuwa Serikali yenu itaendelea kuboresha sheria na sera mbalimbali ili mazingira ya kuwekeza kwenye nyumba yaweze kuwa mazuri zaidi. Aidha, tutaendelea kuchukua hatua zitakazowezesha vyombo vya fedha kupunguza riba ya mikopo wanayotoa. Pia, Serikali inasubiri mapendekezo ya Kamati niliyoiunda Dodoma kuangalia namna ya kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini. Naomba makampuni binafsi nayo yajitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi zetu. Sisi tupo tayari kushirikiana nao. Mahitaji ni mengi, Shirika la Nyumba haliwezi kukidhi kiu ya soko la nyumba za gharama nafuu peke yake.
Mheshimiwa Naibu Waziri;
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru nyote mlioshiriki katika tukio hili la kihistoria la uwekaji wa jiwe la msingi katika nyumba za gharama nafuu hapa Kibada. Naona sasa ndoto yangu ya kuwa na nyumba za gharama nafuu nchini inaanza kutimia. Endeleeni kusimamia kwa bidii ujenzi wa nyumba hizi. Nyumba huleta amani ya nchi, hivyo tuendelee kutimiza wajibu wetu kwa kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanamudu kuwa na makazi bora.
Baada ya kusema hayo sasa napenda kutamka rasmi kuwa niko tayari kuweka jiwe la msingi la nyumba za gharama nafuu hapa Kibada, ikiwa ni ishara ya kuzindua miradi mingine ya aina hii inayotekelezwa na Shirika katika maeneo mbalimbali nchini. Wananchi watumie fursa hii vizuri. Nyumba zipo zinaendelea kujengwa nchi nzima.