Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ndugu Irene Charles Isaka kufuatia kifo cha ghafla cha Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Bwana Siraju Juma Kaboyonga.
Marehemu Kaboyonga ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amefariki ghafla usiku wa kuamkia 19 Desemba, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Bwana Siraju Juma Kaboyonga ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambako amefanya kazi kwa muda mfupi kabla mauti hayajamkuta”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Nilimfahamu Marehemu Siraju Juma Kaboyonga, enzi za uhai wake, kama Kiongozi na Mtumishi mwenye uwezo mkubwa aliouonyesha dhahiri alipokuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo vipaji vyake alivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia kikamilifu Wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini na kwa kweli Umma wa Watanzania kwa ujumla”.
Rais Kikwete amesema ni uwezo wake huo mkubwa uliomwezesha kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambako hakika mchango wake mkubwa unaonekana dhahiri hivi sasa.
“Kufuatia msiba huu mkubwa, ninakutumia Salamu zangu za Rambirambi wewe Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ndugu Irene Charles Isaka kwa kumpoteza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka yako. Aidha kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu kwa kupotelewa na Kiongozi, na kwa kweli Mhimili madhubuti wa Familia”.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Siraju Juma Kaboyonga. Amewahakikishia wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo huku akiwataka wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.