Dkt Huvisa awajia juu Maofisa maliasili

WAZIRI wa nchi,Ofisi ya makamu wa Rais Mazingira Dkt. Terezya Huvisa amewajia juu maofisa maliasili hapa nchini kwa kushindwa kudhibiti tatizo la uharibifu wa mazingira na kuwakamata wahalifu wa mazao ya misitu na badala yake kuwaachia polisi jukumu hilo.
Dkt. Huvisa aliyasema hayo jana mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mkutano wa asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira mkoani Kilimanjaro ambapo alisema maofiosa hao kama wameshindwa kazi ni vema wakajitoa.
Alisema kwa sasa suala la kawakamata wahalifu wa uharibifu wa mazingira limekuwa ni la polisi ili hali maofisa maliasili na mazingira wapo katika kila halmashauri pamoja na watendaji kata hali ambayo inaonyesha kuwa wamejisahau.
Aidha alisema ni wakati wa watendaji hao kuamka usingizini na kutekeleza majukumu yao ipasavyo badala ya kuendelea kulegalega na kuacha mzigo kwa mtu mmoja ambaye ni mkuu wa mkoa.
“Hivi ni kwanini kamatakamata leo ya uharibifu wa mazingira ni polisi,maofisa maliasili na mazingira wako wapi?alihoji waziri huyo na kuongeza kuwa inakuwaje mkuu wa mkoa apigiwe simu kupewa taarifa za uharibifu wa mazingira ili hali viongozi wengine kuanzia ngazi za kata na hata wilaya wakiwemo maofisa maliasili wapo,ni dhahiri kabisa kuwa mmeshindwa kazi na mnapaswa kujitoa”alisema Dkt. Huvisa.
Katika hatua nyingine Dkt. Huvisa alizitaka halmashauri za wilaya kuchukua jukumu la kuhakikisha kuwa kunakuwepo na vitalu vya miti vya kutosha na shule zote katika halmashauri zinashiriki katika zoezi la upandaji miti.
Alisema ni vema viongozi wote kuanzia wakuu wa wilaya,wakurugenzi na watendaji wa kata kila mmoja akatekeleza wajibu wake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya dhati ya kurudisha uoto wa asili katika hali yake ya awali.
Awali akizungumza mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama alisema pamoja na jitihada ambazo zinachukuliwa na mkoa huo ili kuhakikisha unadhibiti tatizo la uharibifu wa mazingira bado kumekuwepo na watendaji wa vijiji na kata ambao wameendelea kuvifumbia macho vitendo vya uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.
Bw. Gama alisema tatizo la uharibifu wa mazingira katika mkoa wa Kilimanjaro bado ni changamoto kubwa ambayo imesababisha athari mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa vipindi virefu vya ukame vinavyoambatana na upungufu mkubwa wa mvua pamoja na kupungua kwa theluji katika mlima Kilimanjaro hali ambayo inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii.