HARARE, ZIMBABWE
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal Jumatano Aprili 29, 2015, ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa dharura wa Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Harare, chini ya Uenyekiti wa Rais Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa sasa wa SADC pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Mkutano huo wa siku moja pia umehudhuriwa na Rais Seretse Ian Khama, Rais wa Botswana na Makamu Mwenyekiti wa SADC, Mfalme Muswati III wa Swaziland, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, Rais wa Namibia Hage Geingob, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa Lesotho Pakalitha Mosisili, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Rais wa Zambia Edgar Lungu.
Awali akifungua mkutano huo Rais Mugabe alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kuwa na mpango madhubuti wa Viwanda kwa kuwa uwepo wa viwanda utasaidia kupunguza tatizo kubwa linalozikabili nchi hizi hasa ajira, pamoja na uchumi duni unaotokana na ukosefu wa viwanda vya kuboresha bidhaa zinazozalishwa katika nchi za ukanda huu. Mkakati huu uliopitishwa na Wakuu wa nchi na Serikali wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaanza mwaka huu 2015 hadi mwaka 2063. Katika mkakati huu nchi za SADC zinalenga kutanua uhuru wa soko katika utatu wa kanda za Kibiashara yaani SADC, EAC na COMESA ikiwa ni pamoja na kutenga eneo huru la ukanda wa kiuchumi wa nchi za kanda hizi, huku lengo likiwa kufanikiwa upatikanaji wa eneo huru la ukanda wa biashara kwa nchi za Afrika. Masuala mengine ni pamoja na kukuza bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizi katika masoko ya Asia ambao ni walaji na watumaji wakubwa wa malighafi zinazozalishwa katika nchi hizi.
Rais Mugabe alifafanua pia kuwa, nchi hizi kwa umoja wake zikiunganishwa utakuta ndizo zina rasimali kubwa ya madini ya Dhahabu, Almasi na hata Gesi na kwamba kama mtengamano huu utakamilika nguvu ya pamoja inaweza kugeuza hali ya maisha ya wananchi wa nchi hizi sambamba na maendeleo ya kiuchumi katika nchi hizo.
Awali akizungumza kabla ya hotuba ya ufunguzi ya Rais Mugabe, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stargomena Lawrence Tax aliishukuru serikali ya Zimbabwe kwa maandalizi mazuri ya mkutano huu ambao ulikuwa ni mwendelezo wa ule uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe Agosti 17, 2014 mkutano uliotaka nchi wanachama wa SADC pamoja na kupitisha mkakati wake wa Kimaendeleo, upange dira ya utanuaji na uendedlezaji viwanda katika ukanda huu.
Matukio mengine katika mkutano huu ni pamoja na makabidhiano ya Kituo cha Mafunzo ya Utunzaji Amani katika nchi za SADC, makabidhiano yaliyofanywa na nchi ya Zimbabwe chini ya Rais wake Robert Mugabe kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt Stargomena Tax. Kufuatia makabidhiano haya, Chuo hiki sasa kitakuwa kinamilikiwa na SADC na matumizi yake yatahusisha vyombo na wataalamu mbalimbali wanaohusika na masuala ya utunzaji amani ndani ya nchi hizi, ili kupata mafunzo ya kuboresha kazi zao kufuatia migogoro kuwa mingi katika nchi mbalimbali Afrika.
Pia Rais Mugabe alitumia muda huo kuutaka Mkutano huu wa Dharura kutoa heshima zao kufuatia kifo cha Brigedia Jenerali Hashim Mbita aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Ukombozi kwa kutambua mchango wake katika uhuru wa nchi zilizomo SADC na pia mchango wake kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizi. Raia Mugabe alimtaja Hayati Brigedia Mbita kama mpiganaji mahiri na kiongozi aliyefanya kazi kwa maslahi ya watu wengi bila kuchoka na kwamba Afrika na SADC vitamkumbuka daima kwa mchango wake huo.