DAKTARI binafsi wa Michael Jakson, Dk. Conrad Murray amekutwa na hatia ya kosa la mauaji bila kukusudia na Mahakama moja mjini Los Angeles, Marekani.
Baraza la wazee wa mahakama – wanaume saba na wanawake watano – wametumia siku mbili kujadili kesi na kufikia hukumu hiyo. Taarifa zinazohusiana na kesi hiyo zinasema Michael Jackson alifariki Juni 25 mwaka 2009 kutokana na kuzidisha kipimo cha dawa ya usingizi.
Adhabu
Murray mwenye umri wa miaka 58 anaweza kukabiliwa na adhabu kamili ya kwenda gerezani kwa miaka minne na kupoteza leseni yake ya uganga. Michael Jackson alipanga kurejea jukwaani mwaka 2009
Wanasheria wa Dk. Murray walihoji kuwa Michael Jackson alijidunga mwenyewe dawa hiyo wakati daktari wake akiwa nje ya chumba.
Dk. Murray alipelekwa rumande baada ya kukutwa na hatia na atasalia huko hadi wakati atakaposomewa adhabu yake, inayotarajiwa kutolewa Novemba 29. Akielezea uamuzi wake, jaji alisema Dk. Murray kwa sasa ni mhalifu aliyekutwa na hatia na kwa kuwa anafahamiana na watu nje ya jimbo la California, inamaanisha hakuna uhakika kuwa daktari huyo ataweza kubakia bila kutoka katika jimbo hilo.
Dk Murray alibaki kimya mahakamani hapo, akijisogeza kidogo katika kiti chake wakati hukumu ikisomwa. Maofisa wa mahakama walianza kumfunga pingu daktari huyo wakati jaji akikamilisha kusoma hukumu, na baadaye kupelekwa rumande.
Baraza la wazee – lililoundwa na wazungu weupe sita, Mmarekani mweusi mmoja na Wamarekani watano wenye asili ya Hispania – walijadili shauri hilo kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu asubuhi. Nje ya mahakama, mashabiki wa Michael Jackson walikuwa wakishangilia na kuimba “Hatia! Hatia!” muda mfupi kabla ya hukumu kusomwa.
Wakati wa wiki sita za kusikilizwa kwa kesi hiyo, mashahidi 49 na zaidi ya vipande 300 vya ushahidi viliwasilishwa mahakamani hapo. Michael Jackson ambaye alikuwa kimya katika ulimwengu wa sanaa kwa miaka kadhaa, alikufa mwaka 2009 wakati akijiandaa kufanya mfululizo wa maonesho katika ukumbi wa 02 jijini London.
Katika hoja za mwisho mahakamani siku ya Alhamisi, upande wa mashtaka ulisema Dk Murray alisababisha kifo cha nyota huyo kutokana na uzembe, na hivyo kuwanyima watoto wa Jackson haki ya kuwa na baba.
Upande wa utetezi ulihoji kuwa Jackson alikuwa amejizoesha kutumia dawa, kitu ambacho kilisababisha kifo chake kutokana na kujipa kiwango kikubwa cha dawa ya huku daktari wake akiwa nje ya chumba katika jumba alilokuwa amekodi nyota huyo mjini Los Angeles.
-BBC