Dk. Slaa, Mbowe kuanza mapambano leo Igunga

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilibroad Slaa

Na Mwandishi Wetu, Igunga

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kinatarajia kuzindua rasmi kampeni zake za kumnadi mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga. Dk. Willibroad Slaa, ndiye atakaye ongoza zoezi zima la uzidunzi wa kampeni hizo. CHADEMA katika uchaguzi huo Joseph Kashindye.

CHADEMA imepanga kuzindua kampeni zake katika viwanja vya Sokoine, huku hafla hiyo ikitarajia kuhudhuriwa na viongozi wake wakuu na machachari, Dk. Slaa, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe pamoja na wabunge wote wa CHADEMA.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupitia kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga, Protace Magayane imetangaza kupuuza pingamizi zote ambazo zilitolewa jana na Mgombea wa Chama cha Wananchi (C U F), Leopold Mahona, aliyewapinga wagombea wa CHADEMA na CCM, Dk. Peter Kafumu, akiwatuhumu kuwa hawana sifa kwani wao ni wafanyakazi wa Serikali.

Akifafanuzi zaidi juu ya suala la pingamizi, msimamizi wa uchaguzi huo alisema kwa mujibu wa sheria na maadili ya utumishi wa umma na sababu alizozitoa malalamikaji si za msingi, hivyo pingamizi hilo halina msingi kwani watumishi hao waliomba ruhusa mapema kutoka katika idara zao kwa ajili ya kuingia kwenye mchaguzi.

Alisema mgombea wa CHADEMA alikuwa mtumishi wa Idara ya Elimu Halmashauri ya Igunga na kwa sasa ameacha kazi, na kwamba ofisi husika inatambua suala hilo, huku akiongeza kuwa mgombea wa CCM, naye aliomba ruhusa ya bila malipo.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya CHADEMA zinasema kampeni za chama hicho huenda zikawa tishio kwa wapinzani wake, hasa CCM kutokana na mvuto wa Dk. Slaa kwa umma mkubwa, Mbowe pamoja na wabunge vijana na machachari wa chama hicho.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi ndiyo mpinzani mkubwa wa CHADEMA katika uchaguzi huo, na huenda kikatumia muda mwingi kujibu tuhuma hasa za ufisadi ambazo zinaweza kukigharimu katika uchaguzi huo.

Msimamizi huyo wa uchaguzi, Magayane amewataja wagombea nane walioteuliwa na NEC kuwa ni Kashindye (CHADEMA), Dk. Kafumu (CCM), Mahona (CUF), Steven Makingi (AFP), John Maguma (SAU), Hemedi Ramadhani (UPDP), Hassani Ramadhani (CHAUSTA) pamoja na Said Makeni (DP).