Dk Sheini awaandalia wapiganaji Vikosi vya Ulinzi na Usalama chakula

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Brigedia Jenerali wa JWTZ, Farah Abdi Mohamed, wakati alipowasili katika kambi ya Bavuai huko Migombani nje ya Mji wa Zanzibar jana, wakati alipowaalika Maaskari wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika chakula cha Mchana.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana aliungana na viongozi anuai katika chakula maalum alichowaandalia Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara Maalum za SMZ walioshiriki katika Gwaride la Maadhimisho ya Miaka 48 ya Mapinduzi.

Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Kambi ya Jeshi Bavuai, mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri pamoja na Wakuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wengine Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akimkaribisha Rais Dk. Shein katika Kambi hiyo ya Bavuai, Brigedia Jenerali Farah Abdi Mohammed alitoa shukurani kwa niaba ya vikosi vyote vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuandaa chakula kwa ajili ya washiriki wote wa gwaride la maadhimisho ya Miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Brigedia Jenerali Mohammed ambaye pia, ni Kamanda wa Brigwdi ya 101, alieleza kuwa hatua hiyo ya Dk. Shein kuwaandalia chakula na kula nao pamoja kwa lengo la kuwapongeza kutokana na kushiriki vyema katika sherehe za kutimiza miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar imewapa faraja kubwa na wametambua jinsi viongozi wao walivyokuwa nao karibu katika masuala ya ulinzi na ujenzi wa Taifa.

Alisema kuwa mbali ya shughuli hizo Jeshi hilo pia, lina kazi ya ulinzi wa Zanzibar pamoja na shughuli za uokozi, majanga na maafa ya kitaifa, mapokezi ya wageni mashuhuri wanaotembelea Zanzibar pamoja na shughuli nyenginezo.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Dk. Shein, mara baada ya chakula hicho maalum, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, alitoa shukurani kwa mwenyeji wa Kambi hiyo Brigedia Jenerali Farah kwa kukubali kuwa mwenyeji wa hafla hiyo.

Dk. Mwinyihaji Makae alitoa pongezi zake na shukurani kwa Vikosi hivyo vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kazi nzuri kwa gwaride la Januari 12, 2012 ambalo lilifanikisha vyema sherehe hizo adhimu.

Akiendelea kutoa shukurani kwa niaba ya Rais, Dk. Mwinyihaji Makame alieleza kuwa vikosi shiriki vyote katika gwaride hilo vilifanya vizuri na watu wote waliridhika na kutoa shukurani zake za dhati kwa gwaride hilo la mwaka huu kwa niaba ya Dk. Shein. Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alivieleza vikosi hivyo kuwa hivi sasa maandalizi makubwa ni kwa ajili ya kufanya matayarisho ya miaka 49 na miaka 50 ya Mapinduzi lakini matayarisho makubwa hasa ni yale ya kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12. 1964.