Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akishiriki katika uzinduzi wa Uvunaji wa Mpunga wa mbegu, aina ya NERICA, huko katika shamba la kilimo la Mbegu hiyo Bambi Mkoa wa Kusini Unguja jana. (Picha na Ramadhan Othman, IKULU)
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali
Mohamed Shein amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la
kufanya Mapinduzi ya kilimo tayari limeanza kutekelezwa na mbegu ya aina
ya NERICA ndio mkombozi wa kufikia lengo hilo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti mara baada ya
kushiriki kikamilifu katika uvunaji wa mbegu ya mpunga wa kilimo cha juu
aina ya (NERICA) huko Bambi na uzinduzi za uvunaji mpunga Kitaifa,
huko katika bonde la Kisimamchanga Kiboje Mkwajuni Wilaya ya Kati Mkoa
wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa mbegu ya aina ya NERICA ni
mkombozi mkubwa katika kufikia malengo yaliokusudiwa katika Mapinduzi ya
Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula.
Alisema kuwa Serikali kwa upande wake tayari imeshaanza kutekeleza
Mapinduzi ya Kilimo kwa kuamini kuwa hatua hiyo ni moja ya kupambana na
mfumko wa bei ya vyakula hasa mchele ambao ndio chakula kikibwa hapa
Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa ongezeko la idadi ya watu hapa Zanzibar tokea
Mapinduzi Matukufu ya Januari mwaka 1964 ambapo idadi ya watu ilikuwa ni
laki 3 na mnamo mwaka 1974 ilikuwa ni laki 640 elfu na sensa ya mwaka
2002 idadi ikafikia milioni 1.2 hatua ambayo nayo imepelekea maongezeko
ya mahitaji yakiwemo chakula.
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuongeza
uzalishaji wa chakula kwani kwa mujibu wa takwemi inaoneshakuwa mchele
unaotumiwa kwa chakula hapa Zanzibar ni tani 80 elfu lakini
unazozalishwa na wakulima hapa nyumbani ni tani 16 elfu tu na kiasi
chote kilichobaki hununuliwa nje ya nchi, ‘Hii ni mbegu na yule atakae
piga goti ale basi ataharibu”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein aliwataka wakulima nao kubadilika na kushirikiana
vizuri na wataalamu wa sekta ya kilimo katika kuhakikisha mbegu hiyo ya
aina ya NERICA inaleta tija kwa wakulima na wananchi kwa jumla na
kusisitiza nia ya serikali ya kubadilisha mfumo mzima wa kilimo kwa
kutumia vifaa na nyenzo za kisasa za kilimo ili kuondokana na kilimo cha
kilichopitwa na wakati.
Alisema kuwa serikali kwa mara ya kwanza italeta mashine za kuvunia
mpunga ili wakulima wapate kuvuna kwa tija kwani ni njia moja wapo ya
kuimarisha sekta ya kilimo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa mikakakti madhubuti
iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake ya
Kilimo ni kuhakikisha wakulima wanapatiwa mbegu bora, mbolea,
pembejeo, Mabwana Shamba, huduma ya umeme na maji ya kutosha.
Dk. Shein alisema kuwa tayari washirika wa maendeleo nao wanaendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika sekta hiyo wakimo Japan, Korea ya Kusini,
Marekani hasa katika mradi wao wa ‘Feed the future’ na wengineo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali imedhamiria kukiimarisha kilimo
cha aina zote likiwemo zao la karafu, pilipili na nyenginezo pamoja na
kuimarisha mbegu mpya ya muhogo ambayo ipo na kuwaahidi wakulima kuwa
watapewa.
Akiwa katika bonde wa Kisimamchanga akizungumza na wakulima wa bonde
hilo, alitoa pongezi kwa wakulima hao kwa jitihada zao za kuendeleza
kilimo cha mpunga kwa kuongeza mara nne uzalishaji wa mpunga katika
bonde lao kutoka na mradi wa PADEP.
Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana
pamoja na wakulima hao katika kufikia lengo hilo “Ili tule ni lazima
tulime”,alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa tayari serikali imeshapitisha Sheria ya Usalama wa Chakula
hivi karibuni kwa kuzingatia umuhimu wa uhifadhi wa chakula ambapo
serikali itajenga mahala ya chakula kwa lengo la kuweza kusaidia pale
patakapotokezea uhaba wa chakula.
Pia, Dk. Shein akiwa katika bonde hilo aliwaahidi wakulima hao
kuwajengea njia yao inayotoka barabara kuu hadi bondeni kwa kiwango cha
kifusi, umeme, kuchimbiwa kisimatela la kubebea mizigo, mashine za
kuvunia na iwapo wataalamu watahsuri kujengwa hala la kuhifadhi mpunga,
pia, serikali itajenga.
Naye, Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe. Mansour Yussuf Himid aliwaeleza
Wakulima kuwa katika Bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2011-2012 itakuwa na
matumaini makubwa na kuleta faraja kwa wakulima wote wa Zanzibar.
Alisema kuwa miongoni mwa malengo na matarajio ni kuhakikisha bei ya
mboleo, mbegu, huduma za matrekta, dawa za kuulia wadudu bei zake
zitakuwa ndogo sana kwani serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein
ameshakisikia vilio vya wakulima juu ya bei za mahitaji hao.
Alisema kuwa dhamira ya Wizara ya Kilimo ndani ya miaka mitano ni kulima
hekta 6000 za umwagiliaji maji ndani ya hekta 8521 ambapo kati ya hizo
ni hekta 700 tu ndizo inzolimwa hivi sasa na kueleza kuwa tayari Korea
ya Kusini katika mradi wake italima hekta 2000 na Marekani hekta 2000.
Aidha, alisema kuwa mashamba darasa yataongezwa na kufikia 1200, ambapo
pia mashaba darasa nne za mikarafuu zikiwemo mbili za Unguja na mbili za
Pemba zitaanzishwa ikiwa ni pamoja na kuazishwa kwa mradi mpya utaoweza
kuwakopesha wakulima fedha sanjari na kuliimarisha bonde la Kibonde
Mzungu ili kuweza kuzalisha mbegu za mpunga.
Pia, Mkuu wa Mkoa aliwatoa hofu na kuwataka wakulima wa Bonde la
Kisimamchanga kuendelea kulitumia bonde hilo ambapo tayari limeshapimwa
na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuanza kilimo cha umwagiliaji maji.
Nao wakulima wa bonde la Kisimachanga walieleza kuwa mara baada ya
kuingia katika mradi wa PADEP ambao umetumia zaid ya Shilingi milioni 32
mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa
mpunga ambapo hivi sasa wanazalisha polo 4 kwa robo hekta ambazo hapo
zamani ndizo walizokuwa wakizalisha kwa hekta nzima.
Katika hafla hiyo ya kitaifa baadhi ya wakulima na viongozi kutoka mikoa
yote mitano ya Unguja na Pemba walihudhuria pamoja na Mawaziri,
Wawakilishi, Mkuu wa Mkoa wa Kusini ambaye n mwenyeji pamoja na Mkuu wa
Mkoa wa Mjini Mgharibi na Kusini Pemba walihudhuria, viongozi wa
serikali na kisiasa, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali
walihudhuria.
Jumla ya heka tano za mbegu ya mpunga wa aina ya NERICA zimevunwa pia
mbegu hizo zinatarajiwa kupandwa kwa wingi katika mvua za vuli
zinazokuja kwa lengo la la kuja kupandwa wakati wa Masika ambapo zaidi
ya tani 3700 za ziada zinatarajiwa kupatikana katika msimu wa masika
ujao lengo ni kufikia asilimia 50 ya uzalishaji ndani ya miaka mitano.