Dk. Shein kufunga Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za kufunga michuano ya 35 ya CECAFA Tusker Challenge Cup inayoendelea jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF leo Dar es Salaam, sherehe za ufungaji wa mashindano hayo yaliyoshirikisha mataifa 10 wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na timu mbili mwalikwa zitafanyika Desemba 10 mwaka huu baada ya mchezo wa fainali utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakati huo huo, aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Robert Jama Mba ambaye ni raia wa Cameroon ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili acheze soka nchini humo. Shirikisho la Mpira wa Miguu Cameroon (FECAFOOT) limetuma maombi hayo jana (Desemba 5 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kupata hati hiyo.

Mba ambaye aliichezea Yanga enzi za uongozi wa Imani Madega ameombewa ITC kwa ajili ya kujiunga na klabu yake ya zamani ya Tiko United baada ya mkataba wake ndani ya Yanga kumalizika. TFF inafanyia kazi maombi hayo na ITC itatolewa wakati wowote baada ya taratibu husika kukamilika.