Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WATENDAJI na Viongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati wameeleza kuwa uwekaji waya wa umeme unaopita chini ya bahari umekamilika na sasa umekaribia kufika Zanzibar. Wamesema kukamilika kwa zoezi hilo kutalifanya tatizo la umeme katika kisiwa cha Unguja kubaki historia.
Maelezo hayo yametolewa na watendaji na viongozi hao katika mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa kwenye muendelezo wa mikutano ya kukutaa na watendaji na viongozi wa Mawizara yote ya SMZ katika kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012 pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka 2012-2013.
Mkutano huo umefanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Wizara hiyo ilieleza kuwa utengenezaji wa waya wa baharini wenye kilomita 39.5 umekamilika na hivi sasa uko njia.
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Hassan Ali Mbarouk, aliyasema hayo katika kikao hicho na kueleza kuwa ulazaji wa waya huo wa pili wa chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni hadi Ras Fumba unatarajiwa kufanywa Agosti mwaka huu.
Alieleza kuwa kazi hizo zote zimegharamiwa na MCC, ambapo kwa upande wa matayarisho tayari ukamilishaji wa uwekaji wa transfoma mbili kubwa zenye uwezo wa 60MVA kila moja tayari umeshafanywa.
Uongozi huo ulieleza kuwa ziara ya utafiti katika eneo la mradi kutoka Ubungo hadi Ras Fumba na Ras Fumba hadi Mtoni umeshakamilika kazi ambayo inatekelezwa na Kampuni ya Kalpataru kutoka India.
Kampuni ya VISCAS CORPORATION ya Japan ndio inayotengeneza waya huo pamoja na kuulaza baharini mara utakapofika, ambapo Kampuni ya SYMBION ya Marekani ikishirikiana na Kampuni ya ALSTOM ya Ufaransa ndizo zinazotengeneza vituo vya kupokea umeme.
Uongozi huo ukiongozwa na Waziri wake Ramadhan Abdalla Shaaban ulieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha umeme katika kisiwa cha Unguja ili kwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Mradi wa uwekaji wa waya wa pili wa umeme kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar ni mradi wenywe lengo la kuweka waya wa pili wa umeme wenyewe uwezo wa kuchukua megawati mia moja (100 MW). Mradi huo ulianza utekelezaji wake Julai mwaka 2008 na unatarajiwa kukamilika miezi ya mwanzo ya mwaka ujao.
Uongozi huo ukieleza kuhusu suala la ardhi, ulisema kuwa sekta hiyo inajukumu la kuhakikisha kunakuwepo Mipango bora ya Matumizi ya ardhi katika ngazi tofauti, kufanya usajili wa ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi inayojitokeza.
Kwa upande wa maendeleo ya makaazi, uongozi huo ulieleza kuwa Dira ya 2020 inaelekeza mkazo suala la upatikanaji wa makaazi bora na kuondokana na matatizo ya makaazi yasio ridhisha pamoja na kuimarisha usimamizi wa miji na vijiji kutokana na ongezeko kubwa la watu.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza kuwa sekta ya maji ina dhima ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watu wote na sekta zote kwa kutumia teknolojia ya usimamizi na uhifadhi wa vyanzo vya maji ili kukuza maendeleo ya wananchi kiuchumi na kijamii.
Ukielezea kuhusu Dira ya Maendeleo ya 2020, Wizara hiyo ilieleza kuwa inakusudia kuhakikisha upatikanaji wa Nishati ya kutosha na endelevu yenye kujali mazingira salama kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Wizara hiyo pamoja na mambo mengineyo ilieleza bajeti yake pamoja na vipaumbele na malengo iliyojiwekea sanjari na azma yake ya kuondosha changamoto inazozikabili. Kwa upande wake Dk. Shein alieza haja ya kuongeza bidii katika kufikia malengo yaliokusudiwa na Wizara hiyo.