Na Rajab Mkasaba, Ras-Al-Khaimah
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na mwenyeji wake Kiongozi wa Ras-Al-Khaimah, Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi na kufanya mazungumzo yaliolenga kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande hizo.
Mazungumzo hayo yaliofanyika katika Kasri ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi lililopo mjini Ras-Al-Khaimah, viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya kukuza uhusiano na kuimarisha mashirikiano katika kuinua seka za maendeleo ikiwemo uwekezaji, biashara, viwanda, elimu, Maeneo huru ya Uchumi, Afya na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Aidha, viongozi hao walizungumza juu ya maendeleo katika kuimarisha ushirikiano kwenye sekta nzima ya maeneo huru na uwekezaji sanjari na bandari huru. Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na mwaliko wake na kumpongeza mwenyeji wake kwa mafanikio alioyapata kwa kipindi kifupi. Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras-Al-Khaimah.
Naye Kiongozi huyo alisema, Ras-AlKhaimah itaendeleza ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo. Dk. Shein alisema Zanzibar na Ras-el-Khaimah zina historia kubwa katika nyanja ya kibiashara hivyo hatua zaidi zitaimarishwa kwa pamoja katika kukuza sekta hiyo pamoja na sekta ya uwekezaji.
Wakati huo huo Zanzibar na Ras-Al-Khaimah imesaini Mkataba wa Makubaliano juu ya Ushirkiano katika sekta mbali mbali za maendeleo, saini hiyo ilishhudiwa na Rais Dk. Shein pamoja na Sheikh Saud Bin Al Qasimi huko katika ukumbi wa Kasri ya Sheikh Saud.
Kwa upande wa Zazibar Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman alisaini ambapo kwa upande wa Ras-Al-Khaimah aliyetia saini ni Sheikh Abdalla Bin Humaid Al Qasimi.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na kuendeleza Maeneo Huru ya Uchumi, Bandari Huru ambapo itaifanya Zanzibar kuwa Kituo Kikuu cha Biashara, ushirikiano wa kitaalamu, kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu katika nyanja za afya, nishati, huduma za afya, ufundi.
Aidha, utafiti juu ya vianzio vya maji, mashirikiano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwawezesha wananchi Kiuchumi na kuendeleza ajira pamoja na mambo mengineyo. Pia, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara wa Ras-Al-Khaimah na kueleza kuwa muendelezo wa biashara kati ya Zanzibar na Ras-Al-Khaimah ndio msingi kubwa ya uhusiano uliopo.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kupata maelezo kutoka kwa Jumuiya ya Wafanyabishara wa Ras-Al-Khaimah. Alieleza kuwa ziara hiyo imelenga katika kukuza uhusiano wa kibiashara, viwanda, uwekezaji kati ya Ras-Al-Khaiman na Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vivutio vingi vya Utalii ambapo juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuiimarisha sekta hiyo. Dk. Shein alieleza kuwa ziara hiyo ni ya kidugu na inaimarisha zaidi historia ndefu baina ya Zanzibar na watu wa Ras-Al-Khaiman.
Wakitoa maelezo yao wafanyabishara hao walieleza kuwa Ras-Al-Khaimah ina mambo mengi ya kushirikiana na Zanzibar na kusisitiza kuwa iko tayari kuendeleza uhusiano na udugu wao kwa kuimarisha sekta za maendeleo.
Walieleza kuwa miongoni mwa sekta ambazo wako tayari kushirikiana ni pamoja na sekta za uwekezaji, viwanda, biashara na nyenginezo na kusisitiza kuwa Zanzibar imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya Utalii, hivyo nao wana mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar.
Dk. Shein akiwa na ujumbe wake pia, alitembelea Chuo Kikuu cha Sayansi cha Ras-Al-Khaiman, Hospitali ya rufaa ya Ras-Al-Khaiman pamoja na kutembelea kiwanda cha dawa cha JULPHAR, alitembelea Maeneo Huru ya uwekezaji RAKIA ambako huzalisha bidhaa mbali mbali zikiwemo tiles, vyombo vya nyumbani na vyenginevyo.