RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amezindua Bohari ya Dawa na kueleza kuwa uimarishaji wa huduma za afya lazima uendane na upatikanaji wa dawa ambazo zimetunzwa kwenye mazingira yalio bora na salama.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar katika ufunguzi wa Bohari Kuu ya Dawa, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe ya kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa sasa imepatikana sehemu muwafaka ya kuhifadhia dawa huku akieleza jinsi alivyofarajika na taarifa kwamba kompyuta inayoweka kumbukumbu imeweka programu ya ‘M-supply’ ambayo inawezesha kurahisisha taarifa za hali ya dawa kutoka Hopsitali na vituo vyengine vya afya nchini.
Alieleza kuwa kwa namna hiyo itakuwa ni rahisi kuratibu usambazji wa dawa katika vituo husika na kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa dawa katika vituo husika na kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa dawa mbali mbali kwa wananchi.
Dk. Shein alisisitiza kuwa kwa mfumo huo Serikali itafanya juhudi zake zote katika kuhakikisha fedha zitakazohitajika kwa kununua dawa zinapatikana ikiwa ni pamoja na fedha kwa ajili ya chakula bora kwa wagonjwa sanjari na ufanyaji tafiti mbali mbali.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara ya Afya wajue kuwa watakuwa na kazi ya kubwa ya kufanya ili kutambua ni dawa gani zinahitajika kununuliwa pamoja na kiwango chake kinachohitajika. Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia pia, kuelewa gharama za dawa zinazohitajika ili iwe rahisi kwa serikali kununua dawa hizo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali inajiandaa kununua vifaa na dhana nyengine kwa ajili ya kuwafundishia madaktari bingwa wa Zanzibar ili kupunguza idadi ama kuondosha kabisa mfumo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaifanyia kazi changamoto ya Bajeti ya dawa ili kuhakikisha dawa za kutosha zinanunuliwa.
Dk. Shein pia, alitoa shukuranikwa Serikali ya Maprekani na Serikali ya Denmark kwa misaada mbali mbali wanayoitoa kwa Zanzibar na hasa katika ujenzi wa Bohari hiyo ya Dawa pamoja na kusaidia katika upatikanaji wa dawa muhimu.
Kwa upande wa Wizara ya Afya, Dk. Jidawi alitoa pongezi zake kwa uonozi, watendaji na wafanmyakazi wote wa Wizara hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika sekta ya afya wakati Zanzibar inatimiza miaka 49 ya Mapinduzi matukufu.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Sira Mwamboya alieleza kuwa kuna kila sababu ya kujivunia kwa kua na Bohari hiyo ya Dawa ya kisasa, ambapo kuwepo kwake kumepelekea uwezo wa kuhifadhi dawa nyingi kwa wakati mmoja.
Alieleza kuwa kuwepo na mazingira mazuri ya utendaji wa kazi katika kutunza na kusambaza dawa kupitia mpango wa Zanzibar Integrated Logistic System (ZILS). kutawezesha hospitali na vituo vya afya kuagiza aina ya dawa wanazohitaji kulingana na matatizo ya sehemu zao.
Aidham kwa kutumia utaratibu wa M-Health, taarifa za dawa kutoka katika mahospitali na vituo vyote vya Zanzibar zinaweza kupatikana pamoja na hospitali na vituo navyo vitaweza kufahamu ni dawa ganizilizoko Boharini kwa kipindi hicho.
Alieleza kuwa utaratibu huo umeanza kutumika katika hospitali ya Mnazi mmoja kama ‘pilot’ na baada ya kutathmini matokeao yake na kurekebisha mapungufu yatakayojitokeza ndipo utakapotumika katika Zanzibar nzima.
Mapema Balozi wa Marekani, Alfonso Lenhardt alieleza kuwa Marekani inathamini sana uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya.
Naye Naibu Balozi wa Denmark Bwana Steen Sonne Andersen alieleza kuwa Denmark kupitia Shirika lake la DANIDA limeanza muda mrefu mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Wizara ya Afya.
Akitoa maelezo yake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Saleh Mohammed Jidawi alieleza kuwa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 1. zimetumika katika ujenzi wa Bohari hiyo ambapo Marekani ilitoa asilimi 50, na DANIDA ilitoa asilimia 50 ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechangia zaidi ya Shilingi milioni 500. Viongozi mbali mbali wa vyama na serikali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.