Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutoa elimu kwa wananchi juu ya tatizo la upungufu wa maji katika vianzio vyake pamoja na kueleza athari zinazosababishwa na hali hiyo na kupelekea baadhi ya maeneo kukosa huduma ya maji.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ziara yake ya kutembelea miradi na shughuli mbali mbali zilizo chini ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), ikiwa ni pamoja na kutembelea kituo kikuu cha maji katika matangi ya Saateni, chemchem ya Mwanyanya, tangi la Dole, visima vya maji kizimbani, matangi ya maji Welezo na chemchem ya Mtoni.
Katika ziara yake hiyo Dk. Shein alipata maelezo mbali mbali kutoka kwa uongozi wa ZAWA katika maeneo aliyotembelea na kuelezwa mikakati iliyowekwa na Mamlaka hiyo pamoja na changamoto zilizopo, ambapo Dk. Shein alisisitiza wananchi kuelezwa hali hiyo pamoja na mikakati iliyowekwa na serikali katika kupata huduma ya maji.
Miongoni mwa changamoto alizoelezwa Dk. Shein na uongozi wa Mamlaka hiyo ni pamoja na kuwepo tatizo la upungufu wa maji katika viazio vyake mbali mbali kutokana na sababu tofauti ikiwemo ujenzi katika maeneo ya vianzio vya maji.
Kutokana na maelezo hayo, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa mbali na changamoto hizoi zilizopo pamoja na mafanikio yaliopatikana kutokana na juhudi za Mamlaka hiyo kuna kila sababu kuwaeleza wananchi juu ya sababu zinazopelekea huduma ya maji kuwa pungufu katika maeneo yao.
Alieleza kuwa sio wananchi wote wanaolewa kuwa kutokana na uvamizi wa ujenzi katika maeneo ya vianzio vya maji kumepelekea huduma hiyo kupungua na kwa baadhi ya maeneo kukosekana kabisa.
Dk. Shein aliendelea kueleza kuwa kuna haja kwa Mamlaka hiyo kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari na kuwaeleza wananchi juu ya hali hiyo ambayo mbali na uvamizi wa maeneo ya vianizo vya maji pia kunatokana na ongezeko la watu sanjari na hali ya tabia nchi hivi sasa.
Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Mamlaka yake ya Maji (ZAWA), juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa uhakika zaidi siku za usoni.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya uhifadhi zadi katika maeneo ya vianzio vya maji kwa kuyawekea uzio na kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo muhimu.
Nao uongozi wa ZAWA, ulimueleza Rais Dk. Shein kuwa miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Mamlaka hiyo juu ya kuhakikisha huduma hiyo inaimarika ni pamoja na kuongeza idadi ya visima na kuimarisha mfumo wa maji.
Uongozi huo pia, ulimueleza Dk. Shein kuwa uzalishaji wa maji katika vianzio vyake umeshuka kutokana na sababu mbali mbali hasa ujenzi katika maeneo ya vianzio vya maji ambao hupelekea kiwango cha maji kupungua.
Sambamba na hayo,uongozi huo ulieleza kuwa mradi wa mkubwa wa maji unaofadhiliwa na serikali ya Japan unaenda vizuri ambapo kwa hivi sasa umo katika awamu ya pili ambapo awamu ya tatu itahusisha kubadilisha mamomba machakavu na kuwekwa mapya katika maeneo yote ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha uongozi huo ulieleza kuwa awamu hiyo ya tatu ya mradi huo mkubwa itahusisha uimarishaji wa visima 10 viweze kuzalisha zaidi kutokana na hivi sasa uzalishaji wake kuwa mdogo ambapo miongoni mwa visima hivyo ni kisima cha Chunga na Mwembemchomeke.
Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa kuna matumaini makubwa ya tatizo la maji kuwa historia kutokana na juhudi za serikali ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), itaikopesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dola za Kimarekani milioni 21 ambazo zitasaidia kuondosha kabisa tatizo la maji kwa kuihuwisha miundombinu ya maji na kuiwezesha Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ijiendeshe wenyewe kifedha.
Pia, Mamlaka ya Maji Zanzibar ZAWA, iliwataka wananchi kutokana na hayo maji kidogo yanayopatikana ipo haja ya kuyatumia kwa uangalifu na kwa wale wanayoyapata wasisahau wajibu wao wa kuchangia huduma hiyo ili iweze kuendeswa vizuri. Uongozi huo pia, ulipongeza ziara hiyo ya Rais Dk. Shein.
Dk. Shein katika uongozi wake amekuwa akizifuatialia kwa karibu changamoto zilizopo ambazo zinapelekea kukosekana kwa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Ambapo hata katika ziara zake nje ya nchi amekuwa akilizunguzia suala hili ambapo hivi karibuni akiwa ziarani katika nchi za Falme za Kiarabu alilizungumza suala hili wakati alipokutana na Watawala wa Sharjah na Ras Al Khaiman ambao nao waliahidi kumuunga mkono.
Miongoni mwa makubaliano kati yake na Watawala hao ilikuwa ni pamoja na kushirikiana katika kufanya utafiti wa vianzio vipya ya maji ambapo wataalamu watapitia kumbukumbu za utafiti uliofanyika Zanzibar miaka iliyopitita. Pia, wataalamu wa maji kutoka Sharjah watatembelea Zanzibar kwa lengo la kufanya utafiti mpya wa vianzio vya maji yanayosemekana kuwepo kwa wingi chini ya ardhi ya Zanzibar.
Sambamba na hayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitia saini Waraka wa Mafahamiano (MOU), huko Ras Al Khaimah ambapo miongoni mwa makubaliano ni pamoja na kushirikiana katika kuviendeleza vianzio vipya vya maji.