Na Rajab Mkasaba, Ikulu- Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Watanzania hasa Wazanzibari kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujiandikisha ili kupata kitambuilisho cha Taifa na kusisitiza kuwa zoezi hilo lisihushihswe na mambo ya siasa. Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la Utangazi la Zanzibar kupitia televisheni, ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu mjini Zanzibar.
Dk. Shein alisisitiza kuwa zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa lisihushishwe na mambo ya siasa kwani hilo ni jambo la serikali na kuwataka viongozi wote katika jamii wakiwemo viongozi wa kisiasa kushirikiana pamoja katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa. Alisema kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kutawapelekea wananchi kupata vitambulisho vyao vya Taifa ambavyo vitawawezesha kujilabu kuwa wao ni Watanzania.
“Wanananchi msihadaiwe wala msidangaywe na mtu yoyote kwani vitambulisho hivyo vitakusaidieni kukutambulisheni Utanzania wenu,” alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema kuwa hiyo ni fursa ya pekee na ana amini kuwa wananchi wote watajitokeza kwa wingi ili kupata haki yao hiyo ya msingi kwa lengo la kupata tija katika maendeleo yao na faida kwao na nchi nzima kwa ujumla.
Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuwaelimisha wananchi kujua umuhimu wa Vitambulisho hivyo huku akiwataka kuwasisitiza kujitokeza kwa wingi kutokana na umuhimu wake mkubwa katika maendeleo ya Mtanzania.
Dk. Shein pia, aliwataka viongozi wa dini wakiwemo Mashekhe na Maaskofu kujitahidi katika kuwaeleza waumini wao juu ya umuhimu wa kujiadikisha kwa kupata vitambulishio hivyo vya Uraia. Pia, alieleza kuwa Masheha, Madiwani na viongozi wa Halmashauri nao wana wajibu wa kusimamia zoezi hilo katika kwa kuhakikisha linakwenda vizuri.
Alisema kuwa vitambilisho vya Taifa vinakidhi matakwa ya Katiba na uraia wa Tanzania na ni jambo la Watanzania wote. Dk. Shein alieleza kuwa suala la vitambulisho vya Taifa ni muhimu kama ilivyo kwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na kusisitiza kuwa vitambulisho hivyo viwili vina sura tofauti.
Alisema kuwa kitambulisho cha Taifa ni kwa ajili ya Uraia wa Tanzania na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ni kwa ajili ya Mzanzibari Mkaazi, vitambulisho ambapo kwa upande wa kitambulisho cha Uraia kinampasa kila Mtanzania kuwa nacho na cha Mzanzibari ni Mzanzibari Mkaazi pekee.
Alieleza kuwa hatua hiyo itawafanya Wazanzibari wawe na vitambulisho viwili ambavyo kila kimoja kitakuwa na matumizi yake kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa upande wa Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.
Akieleza miongoni mwa faida ya kuwa na kitambulisho cha Taifa, Dk. Shein alisema kuwa kitambulisho hicho kitawezesha kuwatambua ni wepi watanzania na ni wepi wageni hali ambayo imepelekea hivi sasa wageni wengi kuutumia msemo wa Zanzibari ni njema atakae aje basi huja na baadae kuhamia bila ya kufuata taratibu za kisheria.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa vitambulisho vya Mzanzibari vitaendelea kutumika kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Zanzibar ambapo imetaka kila mmoja awe na kitambulisho cha Ukaazi. Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Wazanzibari wataendelea kujilabu na kujidai kwa kitambulisho chao cha Mzanzibari Mkaazi.
Alisisitiza kuwa kila kitambulishio ni muhimu na kila kimoja kina kazi na matumizi yake na kwuaeleza wananchi watambue kuwa Serikali imetumia fedha nyingi sana katika kufanikisha zoezi hilo, hivyo wanapaswa washiriki kikamilifu. Zoezi hilo linatarajiwa kuanza tarehe 15 mwezi huu.
Dk. Shein akifungua semina semina elekezi kuhusu Utambuzi na Usajili wa Watanzania kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi huko katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani mjini Unguja Julai, 3 mwaka jana alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipata hasara nyingi kwa kushindwa kuwatambua watu waishio nchini kutokana na kutokuwa na mfumo wa utambuzi na usajili wa watu Kitaifa.
Katika maelezo yake hayo alisema kuwa kutokuwepo kwa mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu kumeiathiri Tanzania kwa kiasi kikubwa sana katika uchumi, masuala ya jamii na usalama. Alisema kuwa athari hizo zinaweza kuwa kubwa zaidi hasa pale Tanzania inapoingia kwenye soko huria la Afrika Mashariki ambapo kwa upande wa Zanzibar nayo inaguswa na kuhusika sana na atahari hizo.
Akizitaja baadhi ya hasara hizo Dk. Shein alisema ni pamoja na wananchi kuendelea kuwa katika umasikini kwa kushindwa kupata mikopo katika benki na taasisi za fedha ambapo alisema faida ya zoezi hilo litawasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Alisisitiza kuwa Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikipata matatizo na malalamiko mengi kwa kushindwa kumtambua mwanafunzi yupi anastahili mkopo na kwa kiasi gani pia, urudishaji wa mikopo hii umekuwa mgumu kwa kushindwa kuwapata wadaiwa mara baada ya kumaliza vyuo na hivyo serikali kupata hasara.
Kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na hasara unaofanywa na raia kutoka nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa msamaha wa Rais, ni wazi kuwa udhibiti wao umekuwa mgumu kutokana na kushindwa kuwatambua.
Alieleza kuwa serikali imekuwa inapata matatizo na kuingia migogoro na wananchi wakati wa mazoezi ya kuwalipa fidia kutokana na kuchukuliwa ardhi au kubomolewa nyumba zao kwa sababu ya kushindwa kumtambua mmiliki sahihi na anachokimiliki.