Dk. Shein awataka watendaji kuwajibika kwa wananchi

Rais wa Serikali ya Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu-Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa kila mwenye dhamana/utendaji kuheshimu dhamana yake kwa kuwajali walio chini pamoja na wale anaowahudumia.

Alisema inasikitisha kusikia baadhi ya wafanyakazi huwatolea maneno yasioridhisha wanaowahudumia, hali ambayo huchangia wananchi kukata tamaa na kuanza kunungunika huku wakiilaumu Serikali yao.

Alhaj Dk. Shein amesema hayo leo katika hotuba aliyoitoa kwenye Baraza la Idd El Hajj, huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete Pemba na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Makungu, Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji Khamis, Mama Mwanamwema Shein Mama Fatma Karume.

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alieleza kuwa nidhamu ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila mwanaadamu na hayo ni miongoni mwa mafunzo ya Ibada ya Hijja na kusisitiza kuwa ufanisi na utoaji wa huduma katika taasisi za hapa nchini hutegemea sana nidhamu.

“Watoa huduma za aina zote lazima waongozwe na nidhamu katika kuwahudumia watu…tukumbuke kwamba kila binaadamu anastahiki heshima … nidhamu katika sehemu ya kazi itafanikisha lengo la Serikali la kuwa na Utumishi Bora ambao utaongeza ufanisi,” alisema Dk. Shein.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana bila ya wananchi wake kuwa na umoja na mshikamano. Alisisitiza kuwa kila mwananchi ajue ana jukumu la kuchangia maendeleo ya nchi hii katika nafasi yake ambapo Mfanyakazi awajibike kwenye ajira yake, mfanyabiashara ahudumie ipasavyo na mkulima atimize jukumu lake kwa kuzalisha chakula kwa wote.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa mafunzo hayo ya umoja yana umuhimu mkubwa wakati huu Zanzibar ikiwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuudhihirishia ulimwengu kuwa Wazanzibari ni wamoja na hatua hii imefikiwa si kwa kubahatisha, bali Wazanzibari wenyewe waliazimia kufanya hivyo.

Alieleza kuwa ni jambo la kutia moyo kuona idadi ya mahujaji wa Tanzania inaongezeka kila mwaka sambamba na taasisi zinazoshuhulikia kuwasafirisha mahujaji,lakini hata hivyo inasikitisha kusikia kuwa baadhi ya mahujaji hupata usumbufu wa kutekeleza Ibada ya Hija kutokana na huduma zisizoridhisha za baadhi ya taasisi.

Kutokana na hali hiyo Dk. Shein aliwasihi wenye taasisi zinazoshughulikia safari za Hijja wawe na mshikamano na siyo mashindano huku akieleza kuwa Mamlaka za kidini zikiwemo Ofisi ya Mufti na Ofisi ya Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali Amana zitaendelea kushirikiana na Taasisi za wasafirishaji Mahujaji ili kuhakikisha kuwa mahujaji wanapata huduma zifaazo kabla na wakati wa safari.

Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwataka wananchi kuitumia vilivyo neena ya mvua za Vuli zilizoanza vizuri kwa kuimarisha kilimo kwani mvua hizo ni nzuri kwa mazao kama vile migomba, mbogamboga, majimbi, chooko na mazao mengine ya vyakula.

Alhaj Dk. Shein, alisema kuwa Serikali imejitayarisha vizuri kuwasaidia wakulima ili kilimo chao kiwe na tija zaidi na kueleza kuwa zaidi ya mabonde 15 Unguja na Pemba yameshatengwa kwa kilimo cha umwagiliaji maji mwaka huu kwani lengo la serikali ni kumudu kuzalisha chakula kwa asilimia 35 katika kipindi cha miaka mitano na pia, kuweza kuwa na chakula cha akiba pindi likitokea jambo lisilotarajiwa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Uislamu unakemea suala la kuidhuru nafsi, iwe kwa kutoa uhai au kuidhuru kwa namna yoyote ile na kueleza kuwa kwa bahati mbaya sana kuna watu wachache ambao wanaendelea kuikiuka amri hiyo kwa kuingiza dawa za kulevya ambazo huwaathiri sana vijana.

Alisisitiza kuwa ni lazima kila mmoja awe na jukumu la kukabiliana na tatizo hilo kwani hilo si jukumu la Serikali pekee yake na kutoa ufafanuzi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamisheni ya Kupambana na dawa za kulevya katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imejipanga vyema kuhakikisha kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya vinafanikiwa.

Dk. Shein pia, alisisitiza suala la usafi wa mazingira hasa katika kipindi hichi cha sikukuu ambayo inafanyika katika kipindi cha mvua na kuwataka wananchi kushirikiana na Halmashauri na Mabaraza ya miji katika kuimarisha usafi hasa maeneo ya mijini kwani Uislamu unahimiza usafi.

Alhaj Dk. Shein alieleza jinsi Serikali ilivyofarajika na jitihada za wakulima kuuza karafuu zao katika vituo vya Shirika Biashara la Taifa (ZSTC), kwani kuna maendeleo mazuri ya ununuzi wa karafuu ambapo hadi sasa Tani 2,058 zenye thamani ya Shilingi za Kitanzania 30.66 bilioni tayari zimeshanunuliwa.

Pia alisisitiza kuwa serikali ina fedha za kutosha za kununulia karafuu na kinyume inavyodaiwa na baadh ya watu kuwa serikali haina fedha. Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa wakulima kuendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali na kuacha kuuza karafuu kwa watu wa magendo.

Dk. Shein alieleza kuwa Sikukuu hii ambayo hutokea mara moja kwa mwaka ni ya kusherehekea kutimiza Ibada ya Hija ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu na kueleza kuwa kitendo cha kusimamisha nguzo hiyo siyo tu kutii amri ya Allah bali pia, ni kusimamisha Uislamu. Alieleza kuwa kitendo cha Muislamu kukubali kutumia sehemu ya mali yake, kuacha familia yake, ndugu na marafiki, akafunga safari hadi nyumba tukufu ya Makka kuitikia wito wa Mola wake ni kitendo cha utii.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kitendo hichi ni kigezo kizuri cha mja kuweka mbele mapenzi ya Mola kuliko mapenzi yake binafsi, Aidha, ni mafunzo kwa watoto kuwatii wazazi wao na pia, wazazi kuwa mfano bora wa vitendo vizuri kwa watoto na kutolea mfano wa Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail.

Akimalizia hotuba yake Dk. Shein, aliwasihi madereva wote kuwa waangalifu katika kuitumia barabara hususan ipindi hiki cha sikukuu kwani barabara ni ya watu wote na kuwataka wananchi nao kuepuka ajaili zisizo za lazima na kuvitaka Vikosi vya Ulinzi na Usalama kuimaisha amani na sala na kuhakikisha sheria hazivunjwi kwa kisingizo cha sikukuu. Mapema asubuhi ya leo Dk. Shein aliungana na wananchi, viongozi na waumini mbali mbali wa dini ya Kiislamu katika sala ya Idd El Hajj, huk katika viwanja vya Gombani Chake Chake Pemba.

Mara baada ya sala hiyo huko katika Ikulu ndogo ya Wete Alhaj Dk. Shein alipata nafasi ya kusalimiana na kupeana mkono wa Idd na Mashekhe, pamoja na viongozi mbali mbali.