Dk Shein awataka wakufunzi wa uwalimu kubadilika

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka waalimu wa ualimu kubadilika katika utoaji wa mafunzo ya elimu, ikiwa ni pamoja na kubuni mbinu mpya za ufundishaji katika kuwatayarisha walimu.

Wito huo ameutoa leo huko Mchanga Mdogo, Mkoa wa Kaskazini Pemba kaika uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu cha Benjamin Willium Mkapa, sambamba na kuziwekea mawe ya msingi skuli 8 mpya za Sekondari zinazojengwa katika Wilaya zote nne za Pemba. Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa lazima walimu wajitayarishe vyema kabla kuingia darasani pamoja na kuwa na maadili mema na uadilifu ili wanaowafunza ualimu waige sifa za mwalimu bora.

“Wazee walisema , ‘Abebwae huangalia kisogo cha mbebaji’ kwa hakika huu si wakati tena wa ‘Chalk and talk’ hatyuna budi tubadilike,” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa uimatrishaji wa elimu nchini lazima uende pamoja na upatikanaji wa walimu bora.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na juhudi za kuzipatia skuli zake walimu bora watakaotoa taaluma bora inayoendana na mahitaji na maadili ya mazuri ya Kizanzibari. Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya Vyuo vikuu vitatu vilivyopo nchini kikiwemo Chuo Cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Tunguu pamoja na Chuo Kikuu cha Elimu kiliopo Chukwani hivi sasa hapa nchini kuna vyo vyawalimu vitatu ambapo viwili viko Pemba na kimoja Unguja.

Pia, Dk. Sheinalitoa wito kwa wananchi, walimu na wanafunzi kuitumia vyema neema hiyo ili kufikia lengo la kuimarisha kiwango cha elimu nchini na kueleza kuwa walimu watakaopata fursa kwenye skuli hixo maalum lazima waoneshe tofauti na wale ambao fursa kama hiyo haijawafikia.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kumkumbusha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali akiwemo msimamizi mkuu wa shughjuli hizi afanye juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa chuo hicho na skuli mpya zilizojengwa na serikali zinatoa matunda yaliokusudiwa na kusisitiza kuwa hata yeye mwenyewe atafuatilia kwa karibu sana kuangalia kama malengo hayo yanafikiwa.

Alieleza kuwa juhudi za kufikisha na kutoa elimu bora kwa wananchi wote sehemu zote nchini pia, ni moja wapo ya hatua za kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 aliyoinadi wakati akiomba ridhaa kwa wananchi ya kuiongoza Zanzibar. Aidha ni jumla ya utekelezaji wa Mpango wa Dunia wa elimu kwa wote ambao Zanzibar na Tanzania kwa jumla imeridhia.

Katika maelezo yake Dk. Shein aliwahakikishia wananci wa Mchangamdogo kuwa kutokana na kuwa tayari eneo hilo kuwa na skuli ya Sekondari na Chuo cha Ualimu pia serikali itaangalia uwezekano wa kujenga Kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Alieleza kuwa madhumuni ya kujenga vyuo hivyo ni kutoa fursa pana zaidi kwa vijana kusomea ualimu ambapo mazingatio ni kuwa mahitaji ya walimu yanaongezeka kila siku kwa skuli za Serikali na watu binafsi sambamba na ongezeko la idadi ya watu nchini.

Dk. Shein alichukua fursa hiyo kwa kuishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo ambao umesaidia sana kuimarisha elimu ya Sekondari na mafunzo ya Ualimu hapa nchini. Alisema kuwa mkopo huo utawezesha kujenga skuli 19 za kisasa za Sekondari katika Wilaya zote za Unguja na Pemba ambazo leo ameziwekea jiwe la msingi sambamba na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo hicho cha Ualimu cha Benjamin Willium Mkapa na kuwapongeza Wakandarasi wote.

Aidha, Dk. Shein aliwaeleza Wananchi wa MchangaMdogo kuwa, kuwepo kwa chuo hicho katika eneo hilo ni heshima kubwa kwao na ni fursa kwa watoto wo kupata nafasi ya mafunzo ya ualimu hapo hapo. Dk. Shein alitoa shukurani kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na watendaji wake kwa kusimamia vizuri ujenzi huo na ukaweza kumalizika mkwa haraka haraka kwa muda uliopangwa.

Ujenzi wa Skuli hizo pamoja na Chuo hicho cha Ualimu unakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania bilioni 1.947, ambapo Dk. Shein alisema kuwa hilo ni jukumu kubwa ambalo serikali imeamua kulibeba ikizingatiwa hali ya uchumi wake. Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban alimueleza Dk. Shein kuwa Wizara ina mpango wa kuandaa hafla kama hiyo ya kuziwekea mawe ya msingi skuli zote ziliopo Unguja ambapo Dk. Shein atafanya shughuli hiyo.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi Mwanaid Saleh, alieleza kuwa jengo hilo la chuo cha Ualimu litakuwa na vyumba vya madarasa 12, ukumbi wa mikutano, maabara 3, za Kemia, Biolojia na Fizikia pamoja na chumba cha Kompyuta, maktaba, cafteria na nyumba za walimu wanawake na wanaume ambazo zitajengwa katika eneo hilo.

Nao uongozi wa Chuo cha Benjamin Mkapa ulitoa pongezi za pekee kwa Serikali ya Mapinduzi Zazibar kwa kujenga chuo hicho cha kisasa ambao ujenzi wake umezingatia kutoa huduma kwa watu wa aina zote na kueleza haja ya kuzungushiwa uzio chuo hicho pamoja na kujengewa msikiti, kituo cha afya na sehemu za michezo. Dk. Shein leo jioni anatarajia kukagua barabara ya Chanjani-Mitamani-Pujini na kuona jinsi ya ujeni wa barabara hiyo unavyoendelea.