Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein,
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wafanyabiashara kujenga imani ya kufanya biashara bila dhulumu ya bei, vipimo wala ubovu wa bidhaa wanazoziuza hasa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Dk. Shein ameyasema hayo wakati akitoa risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu. Alisema Serikali kupitia vyombo na taasisi zake imeandaa mazingira mazuri ya kufanyia biashara za vyakula kwa mwezi wa Ramadhani, hivyo kusisitiza wafanyabiashara nao kuwa na wema katika kipindi hicho chote.
Aliongeza kuwa wauzaji sokoni na mitaani wanatakiwa kutoa ushirikiano katika jambo hili, na kuzitaka manispaa na halmashauri kuongeza bidii katika usafi wa miji. Alhaj Dk. Shein alisema hali ya chakula inaendelea kuwa nzuri kutokana na wafanyabiashara kuongeza na kuagiza bidhaa, hivyo bei za bidhaa hazitarajiwi kupanda bali kushuka kadri mazao yanavyozidi kuingia sokoni.
Alieleza kuwa kutokana na kuimarika kwa biashara ya nje, hasa kutoka Dubai, bidhaa nyingi zinapatikana maduni hivi sasa kwa ajili ya Ramadhani na hata Sikukuu ya Idd El Fitri.
Dk. Shein alisema kuwa nguzo ya Saumu ina nguvu kubwa za kumuongoza mtu awe na tabia njema, uvumilivu na subira ambapo pia, alisisitiza haja ya utulivu, upendo, uvumilivu, umoja na kuwa na subira hata kwa wasio waislamu.
“Haya ni mambo ambayo tunapaswa kuyatafuta kwa nguvu na imani zetu ili tufanikishe Saum yetu…..misingi mikubwa ya mambo hayo ni imani na ihsani, tukiwa na ihsani tutakuwa Waumini na ndivyo tulivyoamrishwa na MwenyeziMungu katika Suratul Baqara, aya ya 183.
Aidha, mbali ya malipo ya saumu kutoka kwa MwenyeziMungu lakini yapo malipo yanayoonekana kila Ramadhani katika jamii ambapolisisitiza haja ya kuimarisha utulivu, upendo, uvumilivu, umoja na kuwa na subira hata kwa wasiokuwa waislamu.
Aidha, alisisitiza wajibu kwa waumini kuhudhuria na kuhimizana kwenda darsa na pia, kuongozana na vijana na watoto ili wapate misingi mizuri ya maisha sanjari na kuzidisha kusoma Qur-an tukufu katika mwezi wa Ramadhani.
“Nimeiagiza Mamlaka ya Maji na Wizara inayoshughulikia maji isimamie kwa karibu zaidi maeneo ya uzalishaji wa maji, upatikanaji na usambazaji, ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika,” alisema Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa pindi tatizo la maji litakuwa kubwa Mamlaka ya maji kwa kushirikiana na wananchi isambaze maji kwa njia ya kutumia magari ili kuwawezesha wananchi kugfunga Ramadhani bila ya kupata usumbufu.
Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa viongozi na wananchi, hasa Masheha kuwa karibu zaidi na Mamlaka ya Maji katika kipindi cha Ramadhanikwa kutoa taarifa ya hali halisi ya maji katika maeneo yao kwa nia ya kufikia lengo la kuwahudumia wananchi wote.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwahimiza wananchi kuheshimu sana maadili ya Ramadhani, zaidi kwa wafanyabiashara wa vyakula, hoteli na mikahawa, aliwasihi kutambua wajiu wao katika Mwezi Mtukuu wa Ramadhani.
“Maadili ya asili ya mwezi huu Mtukufu yanajulikana vyema na ni vizuri tukayaenzi, tukatazane kwa upole na laima yawepo mafahamianolakni kwa uthabiti na dhamira njema,” alisema Alhaj Dk. Shein.