Dk. Shein Awataka Viongozi Kubadilika

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na viongozi.


Baadhi ya Wajumbe wa Semina ya siku tatu ya Kuimarisha Uhusiano Baina ya Viongozi wa Kisiasa na Kiutendaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakisikiliza mada ya mafanikio yaliyopatikana katika ziara za Viongozi na Watendaji wa SMZ Nchini China, iliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]


Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefungua semina ya viongozi na watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuendelea kusisitiza suala zima la kubadilika katika utendaji wao wa kazi kwa lengo la kuiletea maendeleo Zanzibar kwa kutumia uzoefu wa ziara za mafunzo walizozipata baadhi ya viongozi hao nchini China na Malaysia.

Semina hiyo ya siku tatu inayofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort, ina maudhui ya kuimarisha uhusiano baina ya viongozi wa kisiasa na kiutendaji katika Serikali ya Mapinduzi ikiwa na kauli mbiu ya ‘Viongozi lazima tubadilike’.

Alieleza kuwa semina hiyo itasaidia kuangalia tathmini za semina zilizopita pamoja na uzoefu wa safari za kimafunzo nchini China na Malaysia. Nyengine ni Mipango ya Maendeleo ya miaka mitano, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na E-Government kwa viongozi. Lengo ni kuwa mada zote hizo ziweze kufanyiwa kazi ipasavyo katika utekelezaji wa kila siku wa majukumu yao.

Katika maelezo yake ya ufunguzi wa Semina hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika ziara za kimasomo nchini China na Malaysia ambazo viongozi hao waliowengi serikalini walishiriki aliwataka wazitumie ili ziwe chachu ya utendaji na kupanua wigo wa maendeleo hapa nchini.

Dk. Shein pia, alieleza kuwa mbali ya mada hiyo pia, washiriki watapa mada muhimu inayohusiana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ambayo itasaidia kuweka mikakati ya utekekelzaji wa maagizo. Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, kwa kusaidia uendeshaji wa semina hiyo.

Naye Mwakilishi wa UNDP nchini Tanzania, ndugu Philippe Poinsot, alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendesha semina zenye lengo la kuimarsha Utawala Bora na kuahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha maendeleo. Pamoja na hayo, Mwakilishi huyo wa UNDP, alisema kuwa uundwaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kumesaidia sana kuimarisha maendeleo ya Zanzibar katika sekta mbali mbali.

Alisema kuwa semina hiyo itatoa fursa ya kuangalia masuala mbali mbali kwa kina yanayohusu masuala ya msingi yanayojikita juu ya Utawala Bora hapa nchini. Alisisitiza haja kwa viongozi kubadilika na kuonesha njia. Mapema Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alieleza kuwa semina hiyo ni muhimu sana katika suala zima la maendeleo kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akitoa mada ya kwanza katika semina hiyo iliyohusu Mafanikio yanayopatikana katika ziara za viongozi na watendaji Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nchini China, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee alisema kuwa sababu kubwa ya kuichagua China katika ziara hizo za kimasomo ni kutokana na maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii waliyofikiwa haraka nchini humo.

Alisema kuwa China ilikuwa ni moja ya nchi ambayo iko nyuma sana kiuchumi kabla ya mwaka 1949 na miaka 35 iliyopita Tanzania ilikuwa tajiri kwa kiwango cha pato la Taifa ambapo kwa sasa China ni moja kati ya nchi zenye nguvu za kiuchumi na ni nchi ya kwanza duniani yenye mafanikio makubwa.

Vingozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanashiriki akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu, Wakurugenzi, Maofisa Tawala, Mahasibu wakuu wote wa Wizara, Wenyeviti wa Halmashauri za Mikoa na Wilaya pamoja na viongozi wengine wa SMZ.