Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
VIONGOZI wa Serikali za Mitaa wakiwemo Masheha wametakiwa kutojihusisha na migogoro ya ardhi kwani inaathiri maendeleo ya kilimo, utalii na makaazi ya watu na wakati mwengine huathiri hata amani na usalama katika maeneo yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa semina ya siku tatu ya Viongozi wa Serikali za Mitaa, inayofanyika katika hoteli ya Misali, iliyopo Wesha Pemba. Katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa semina hiyo, Dk. Shein alisema kuwa ni bahati mbaya kwamba mara nyingi Masheha na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa ikiwemo Wizara husika, huwa wanajihushisha na migogoro hiyo.
Alisema kuwa kwa hakika migogoro hii inavuruga ustawi wa uchumi pia, kutokana na ukosefu wa maadili pamoja na kutokuzingatia sheria ziliopo kwa baadhi ya watendaji matokeo yake ni kuwanyima haki zao wananchi wanaostahiki na kupelekea kunungunika.
“Katika yatakayozungumzwa hapa ni suala la ardhi, jambo lenye kuleta utata na migogoro katika jamii Unguja na Pemba na pia ijulikane kuwa tatizo hili si la Zanzibar pekee bali ni la nchi nyingi duniani”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa katika mfumo wa utawala wan chi, viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo Masheha na Madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba misihgi ya utawala bora inatekelezwa.
“Kama nilivyosema kule Unguja, nyie hapa ndio mlioko mashinani na mti wenye shina bovu hauwezi kusimama. Kwa kuzingatia haya, tumeamua kuendesha semina hii maalum kwenu ili kukupeni na nyinyi maelekezo na fursa kamili katika kujadili utawala bora,” alisema Dk. Shein.
Dk Shein alisema kuwa Utawala Bora ni kiini cha ustawi wan chi, amani na utulivu wake na kusisitiza kuwa malengo yote ya nchi yakiwemo uchumi na huduma za jamii yanalenga katika kuleta Utawala Bora kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, suala la utawala bora lina umuhimu wa pekee. Pia, alitoa shukuran kwa UNDP kwa kufankisha semina hiyo. Pia, kwa upande wa Masheha na Madiwani wametakiwa kuwa na mashirikiano na uhusiano mkubwa katika kutunza amani na usalama ndani ya shehia zao.
Aidha wameelezwa kuwa ulinzi unaotolewa na vyombo vya dola au Polisi Jamii ambao unawapa usalama wananchi utafanikiwa tu kwa mashirikiano yao na wahusika wengine. Viongozi hao pia, wametakiwa lazima watambue kwamba utekelezaji wa mipango ya maendeleo unaofanywa na Serikali kwa kupitia kwenye Idara na Wizara zake huwa unatekelezwa katika shehia, zikiwemo upelekaji huduma za afya, elimu, maji na nyenginezo.
Pamoja na hayo, viongozi hao aliwataka watambue jukumu jengine kubwa kwao ni kuchangia katika kuendeleza utalii nchini ambao unazidi kuwa tegemeo kubwa la uchumi sekta ambayo pia, imekuwa ikikua vyema kisiwani Pemba. Viongozi hao pia, wamesisitizwa kuzingatia suala zima la utunzaji wa mazingira na usafi katika shehia zao na kuwaleza kuwa ni lazima yawe ni miongoni mwa majukumu yao makubwa.
Aliwaeleza viongozi hao kuwa ukuaji wa majaa na utupaji ovyo wa taka unaendelea katika shehia hasa Wilaya zenye watu wengi kama vile Wete, Chake, Mkoani na Micheweni wakati Madiwani na Masheha wapo. Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kutokana na mafanikio ambayo kila mmoja atahusika nayo ikiwa ni pamoja na kuelewa misingi ya uongozi, utawala bora, maadili, uwajibikaji na umuhimu wake katika utkelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa.
Semina hiyo ni mfululizo wa semina maalum za viongozi na watendaji wakuu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambazo tayari zimeshafanyika ikiwemo ile ya viongozi wa Serikali za Mitaa iliyofanyika Juni 26, mwaka huu kwa upande wa Unguja na leo ni zamu ya Pemba.
Semina hiyo imelenga katika kutoa maelekezo ya Nyanja mbali mbali za uongozi na kiutendaji, ardhi na migogoo yake jambo ambalo si tatizo la Zanzibar pekee bali ni la nchi nyingi duniani,utawala bora,mazingira, maadili, uchumi na utalii kwa wote, usimamizi wa fedha na ununuzi wa vifaa na nyenzo.
Naye, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Matifa (UNDP) nchini Bi Njeri Kamau alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zazibar katika shughuli zake za maendeleo zikiwemo uendelezaji na uimarishaji wa Serikali za Mitaa kwa kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya nchi.
Mapema Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa semina hiyo pia, ina lengo la kuleta maelewao mazuri kati ya viongozi wa Serikali na wale wa Serikali za Mitaa na kuwataka kujenga maelewano mazuri.
Akitoa mada katika semina hiyo, Afisa Mwandamizi kutoa Serikali za Mitaa, Abrahamai Haji Mnoga alitilia mkazo na kueleza kuwa Sheha hana mamlaka juu ya ardhi na kitendo cha kujihusisha na mauzo ya ardhi za serikali ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa.
Alisema kuwa taasisi inayohusika na ardhi za serikali ipo nayo ni Wizara ya ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na kueleza kuwa wajibu wa sheha ni kulinda mali za Serikali na sio kujifanya wadhibiti wa mali hizo kinyume na sheria. Katika semina hiyo, viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim SeifSharif Hamad pamoja na Masheha na Madiwani wote wa Pemba na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa.