Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein jana amewaapisha Mawaziri kufuatia mabadiliko aliyoyafanya kwa kuwabadilisha Wizara baadhi ya Mawaziri hivi karibuni ambapo pia, amemuapisha Mshauri wa Rais Pemba.
Walioapishwa hii leo ni Ramadhan Abdalla Shaaban kuwa Waziri wa Ardhi, Makaazi Maji na Nishati ambaye kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali. Ali Juma Shahuna kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali ambapo kabda ya kiapo hicho alikuwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati mwengine ni Suleiman Othman Nyanga kuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili ambapo kabla ya hapo alikuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum.
Pia, Dk. Shein amemuapisha, Mansour Yussuf Himid kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri Asiekuwa na Wizara Maalum ambapo kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili, Abdillah Jihad Hassan ameapishwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye kabla ya mabadiliko hayo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.
Said Ali Mbarouk ameapishwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ambapo kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambapo pia, Dk. Shein amemuapisha, Sheha Mohammed Sheha kuwa Mshauri wa Rais Pemba.
Hafla hiyo ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Mapinduzi, Pandu Ameir Kificho, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Haji Omar Kheir,
Wengine ni Waziri Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar, Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib, Wakuu wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Washauri wa Rais, Manaibu Waziri, Naibu Mufti Sheikh Mahmoud Wadi, Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wengine.
Dk. Shein alifanya mabadiliko ya kuwabadilisha Wizara baadhi ya Mawaziri ambao aliwateua kushika nyazifa hizo tarehe 02 Aprili mwaka huu.