Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amefungua jengo la Shule ya Sekondari Kitope na kuwataka wanafunzi wote nchini kusoma kwa bidii ili kuepuka kufanya udanganyifu wakati wa mitihani yao.
Dk. Shein aliyasema hayo jana baada ya kufungua jengo hilo ikiwa ni miongoni mwa shughuli za ziara anayoendelea nayo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja aliungana na Mbunge wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Idd katika ziara hiyo.
Katika ziara yake hiyo ambayo jana aliendelea katika Wilaya ya Kaskazini B, Dk. Shein aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuepuka kufanya udanganyifu katika mitihani yao, “Someni kwa bidii ili muepuke kuja kutumia mabomu katika mitihani yenu”, alisisitiza Dk. Shein.
Aliwaeleza wanafunzi haokuwa wazee na viongozi wao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kuwajengea mazingira mazuri ya kujisomea. Dk. Shein aliwapongeza viongozi wa Jimbo hilo la Kitope akiwemo Mbunge, Mwakilishi na viongozi wengineo waliotoa mchango wao kubwa sanjari la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na SIDA, Halmashauri ya Kaskazini B, na Wilaya yake.
Dk. Shein alilipongeza Shirika la Misaada la Sweden kwa mchango wake mkubwa wa Sh. milioni 43.1 na kumpongeza Mbunge kwa kusaidia madawati ya shule hiyo. Na kuipongeza Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Kitope kwa juhudi zao kubwa za maendeleo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa ya maendeleo katika sekta ya elimu tokea Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kueleza kuwa kabla ya Mapinduzi Mkoa huo ulikuwa na skuli tatu tu za msingi ambapo hivi sasa kuna shule za msingi 86.
Alisema kuwa hatua kubwa imefikiwa na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu ikifananishwa na nchi nyengine zinazoendelea. Kutokana na juhudi hizo aliendelea kuisisitiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuendelea kusimamia Sera na Mipango yote ya elimu na kuwataka viongozi wake wasikae maofisini na badala yake wawe karibu na taasisi za elimu na kuwa karibu na vijana.
Pia, aliwataka waalimu kuitumia vyema dhamana waliyopewa kwani wana dhima kubwa katika kuimarisha sekta ya elimu na kueleza kuwa Serikali haitochelea kuwakosa waaalimu wasio simamia maadili na dhama zao. Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna alitoa wito kwa viongozi wa Majimbo wakiwemo wabunge na Wawakilishi kuiga mfano wa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.
Baada ya hapo Rais Dk. Shein alifungua afisi ya Mbunge wa Jimbo hilo iliopo Kitope na kuwaeleza wananchi wa Jimbo hilo kuwa hivi sasa watapata mahala pazuri pa kumuona na kuzunumza na Mbunge wao kwani tayari ameshapata afisi yake.
Mapema Dk. Shein aliweka jiwe la msingi skuli ya maandalizi ya Fujoni na kupongeza juhudi za wazee, wazazi na vionozi mbali mbali waliochangia katika ujenzi huo na kuahidi kutoa mchango wake wa shilingi milioni moja, katika kuendeleza ujenzi huo.
Katika maelezo yake mara baada ya kuweka jiwe hilo la msingi, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuyapima maeneo yote ya skuli za Msingi na Sekondari na baadae wakabidhiwe hati zao ili kuepuka uvamizi. Alieleza kuwa agizo hilo ni lazima lifanyiwe kai na kila taasisi ipatiwe hati yake.”Udongo ni lazima upate ulimaji
Dk. Shein alisisitiza kuwa ni lazima elimu ya maandalizi ikajengewa mazingira mazuri ili watoto waweze kusoma kwa bidii na wawe na maandalizi mazuri ya elimu. Alieleza kuwa ni vizuri vijana wakaekewa utaratibu maalum wa kupewa elimu ikiwemo elimu ya maandalizi kwa lengo la kuweza kupata mafanikio mapema.
Alieleza kuwa Serikali itafanya kila juhudi katika kuhakikisha elimu ya maandalizi inapewa kipaumbele na kuweza kuleta mafanikio makubwa.
Wakati huo huo Dk. Shein aliweka jiwe la Msingi la Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini B na kuzitaka Halmashauri zote nchini kuwa wabunifu katika kukusanya mapato na matumizi katika maeneo yao.