Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein leo amefanya uteuzi wa Viongozi katika Taasisi mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kwa mujibu wa Taarifa iliotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee imeeleza kuwa kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu 56(1)(a) cha Katiba ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali MohamedShein amemteuwa Ibrahim Mzee Ibrahim kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Kabla ya Uteuzi huo Ibrahim alikuwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha Dk Shein kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu 5(1) cha sheria ya Ofisi ya Mufti Namba 9 ya 2001 amemteuwa Sheikh Mahmoud Mussa Wadi kuwa Naibu Mufti.
Pia kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu 3(1) cha sheria ya Vizazi na Vifo Namba 10 ya 2006 Dk Shein amemteuwa Shaaban Ramadhan Abdulla kuwa Mrajis wa Vizazi na Vifo. Ramadhan ana shahada ya sheria.
Aidha kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu 4(1) cha sheria hiyo amemteuwa Bi Fatma Idd Ali kuwa Naibu Mrajis wa Vizazi na Vifo.
Uteuzi huo wote umeanza leo tarehe 14/1/2012