RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inapeleka huduma muhimu kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyo maeneo ya mbali ambapo huduma hizo hazijafika.
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kuizindua skuli ya Msingi Kidagoni, iliyopo Shehia ya Kidoti Jimbo la Nugwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa huduma hizo ni za sekta ya elimu, afya, maji, umeme na nyenginezo ambazo ni muhimu kwa wananchi wa vijijini.
Alisema kuwa hayo yote yanawezekana iwapo wananchi wataanzisha miradi yao ya maendeleo na hatimae serikali kuwaunga mkono.
Wakati huo huo Dk. Shein alizindua SACCOS ya Potoa na kusifu juhudi zao wanazozichukua katika miradi mbali mbali wanayoiendesha zikiwemo ushonaji, ufumaji, uuzaji wa dagaa, kilimo na shuguli nyengine za kimaendeleo.
Aliwasifu kwa kuanzisha afisi yao wenyewe ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi na kufurahishwa na malengo waliyojiwekea ya muda mrefu katika kuikuza SACCOS hiyo ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza watoto wao wakiwemo wanafunzi wa maeneo hayo.
Katika uzinduzi huo Dk. Shein alifanya harambee kwa ajili ya kusaidia SACCOS hiyo ambapo viongozi mbali mbali walitoa ahadi na fedha taslim hapo hapo kiasi cha Tsh. Miloni 6.3 na Dk. Shein alichangia Tsh. Milioni 3.7 na hatimae kufikia milioni 10 taslim fedha ambazo atakabidhiwa mkuu wa mkoa huo ili alizeleke kwenye SACCOS hiyo.
Aidha, Dk. Shein alizindua ukumbi wa mitihani katika skuli ya Pwanimchangani ambapo katika risala yao wananchi wa kijiji hicho walimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi wa jengo hilo hadi ulipofikia umegharimu Tsh. Milioni 7.6 zikiwa zimetoka katika mfuko wa maendeleo wa Jimbo.
Walieleza kuwa ujenzi huo umesimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A kupitia mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo la Matemwe.
ujenzi huo umefanyika baada ya wenyewe wananchi wakishirikiana na viongozi wao wa Jimbo kuona ipo haja kubwa ya kujengwa kwa ukumbi huo hasa kulingana na taratibu za Baraza la Mitihani.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ali Juma Shamuhuna alisema kuwa ujenzi huo una azma ya kuanza utaratibu wa wanafunzi badala ya kufanya mitihani kwenye madarasa wafanye mitihani kwenye kumbi ili kuepuka mambo mbali mbali ya udanganyifu.
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwataka wanafunzi wa skuli hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kufanya mitihani yao bila ya udanganyifu na kuweza kuutumia vizuri ukumbi huo na kuahidi kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali utamaliza ujenzi huo.
Kabla ya kuanza ziara yake, Dk Shein alipokea taarifa ya Mkoa huo wa Kasakazini Unguja na ambayo ilieleza mafanikio na changamoto zilizopo katika Mkoa huo ikiwemo migogoro ya ardhi ambayo mkoa huo ulieleza kuwa iaifanya kazi.
Akiwa katika kijiji cha Nungwi Dk. Shein alitembelea mradi wa kufuga samaki wa aina mbali mbali wakiwemo kasa na samaki wengineo ambapo Dk. Shein alisifu juhudi hizo za vijana hao ambao wameamua kufanya shughuli hizo na kuweza kujiajii wenyewe.
Dk. Shein pia, alikagua vikundi vya wajasiriamali wanaofanya kazi za mikono na kijijini hapo na kuwasifu kwa juhudi zao huku akizitaka Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananachi Kiuchumi na Ushirika pamoja na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kuwatafutia soko wajasiriamali hao ambao wameweza kujiajiri wenyewe.