RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi wa Zanzibar kuimarisha usafi wa mazingira yao hasa katika kipindi hichi ambacho mvua za Masika zimeanza kupiga hodi kwa ajili ya kuepuka maradhi na majanga mbali mbali yanayoweza kutokezea.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa msikiti Maamur, uliopo Kiembesamaki Milimani, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Unguja. Katika hotuba yake, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa kwa hakika mvua ni neema kwa viumbe vyote ikiwemo mimea, wanyama na wanadaamu lakini mvua hizo wakati mwengine huja na madhara yakiwemo maradhi, athari za mafuriko na uharibifu wa miundombinu kadhaa.
Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa, athari zake hutokea kwa watu kutozingatia hatua za tahadhari zikiwemo watu kujenga nyumba kwenye mabonder, kutupa taka kwenye misingi ya maji na kutotilia maanani suala la usafi wa mazingira ya maeneo wanayoishi watu.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa suala zima la kuweka majaa ya taka katikati ya makazi ya watu au skuli pamoja na kutoacha nafasi ya kutosha baina ya nyumba hadi nyumba hali hizo pia huchangia majanga na maradhi kadhaa. “Tumuombe Mola wetu atujaaliye mvua zijazo, ziwe za kheri, salama na rehema”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Alieleza kuwa ingawa taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa zinaeleza juu ya uwezekano wa maeneo haya kupata mvua za wastani na zitakazoambatana na upepo, lakini alitoa wito kwa wananchi kuanza kuchukua hatua za tahadhari ili kuepuka maradhi yanayoweza kuletwa na mvua hizo za masika.
Kutokana na hatua hiyo alizitaka Taasisi zinazohusika kutoa elimu kwa wananchi na ushauri juu ya namna ya kukabiliana na madhara yanayoweza kuletwa na mvua yakiwemo ugonjwa wa malaria kutokana na kuongezeka kwa mazalio ya mbu pamoja na na maradhi ya matumbo.
“Halmashauri za Wilaya na Mabaraza yafanye kila juhudi kuondosha taka hasa wakati huu wa mvua. Aidha, wakulima nao wazitumie mvua hizi kwa kilma mazao ya chakula na biashara kwa kufuata ushauri wa wataalamu wetu juu ya kilimo na mazao yanayostahiki kulingana na mvua hizi”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu wote wenye uwezo kuitumia neema ahiyo waliopewa na Mwenyezi Mungu katika kusaidia kuujenga Uislamu kwa namna mbali mbali ikiwemo kujenga misikiti, kujenga madrasa na kusaidia vifaa mbali mbali vikiwemo mas-hafu, juzuu na kuchimba visima.
Alisema kuwa wale wenye uwezo mkubwa zaidi waanzishe skuli zitakazofundisha elimu ya dini ya Kiislamu nay a sekula sambamba na maadili ya Kiislamu ili watoto wapate maadili mema. Alhaj Dk. Shein alisema kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa misikiti, Waumini wanapaswa kushirikiana katika utunzaji wake na kuihudumia kwa mahitaji yake kama vile maji, umeme na mengineyo.
Alisisitiza kuwa amisikiti itumike kuimarisha uislamu kwa kuendesha darasa mbali mbali na shughuli nyengine kwa mujibu wa mafundisho ya Dini ya Kiislamu.
Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa suala la kuzuka mizozo katika baadhi ya misikiti ni jambo linalowahuzunisha Waumini walio wengi akiwemo yeye na kueleza kuwa jambo hilo si zuri na halina tija linapotokea katika misikiti na katika jamii kwani Waislamu ni ndugu na mizozo ni amali za kishetani.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa pale zinapotokea khitilafu baina ya waumini kwa bahati mbaya, kwa kuzingatia misingi ya dini ya Kiislamu inapaswa kushughulikiwa khitlafu hizo kwa njia za busara na kwa kushauriana kwani mashauriano katika maisha ya binadamu ya kila siku ni jambo la lazima.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alisisitiza haja kwa Waumini wa dini ya Kiislamu kujipanga kwa sifa za uadilifu na uaminifu kwani mara nyingi sifa hizo huenda pamoja na ni sifa muhimu kwa waumini na kwa Wazanzibari ni sehemu ya malezi kwa vizazi.
Pia, Alhaj Dk. Shein, alitoa shukurani kwa mfadhili aliyejenga msikiti huo kwa mchango wake mkubwa aliotoa kwa Waislamu wenziwe na pia kwa kutafuta radhi za Mola wake.
Naye Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi alieleza kuwa mfadhili wa msikiti huo amefuata kazi walizokuwa wakifanya Mitume iliyopita kwa kujenga misikiti kwa ajili ya ibada na kuwataka waumini wa msikiti huo kuutunza na kuzidisha usafi.
Mapema wakisoma risala yao waumini wa msikiti huo walieleza kuwa msikiti huo uliasisiwa mwaka 1983 kwa kujengwa kwa matope na makuti na mwaka 1985 ulitanuliwa kwa matofali na mwaka 1996 uliongezwa tena na baadae mwaka 2011 ulikaribia kuanguka na ndipo alipotokea mfadhili wa mtaa huo na kuamua kuujenga.
Waumini hayo walieleza kuwa mpaka hatua ya uzinduzi wa msikiti huo umegharimu kiasi cha Sh. milioni 170, na kueleza kuwa msikiti huo una uwezo wa kusaliwa na waumini wasiopungua 400 kwa wakati mmoja.
Walisema kuwa muhisani huyo katika ujenzi wa msikiti huo ametia nia ya kuendelea na ujenzi sehemu ya juu ambapo pia, kutakuwa na ofisi na sehemu ya madrasa kwa ajili ya watoto na watu wazima.