Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema katika kuzingatia uzuiaji wa matukio ya maafa na majanga kuna kila sababu wananchi kupewa elimu na kuzifahamu sababu zake ili jamii ipate uelewa zaidi.
Dk. Shein aliyasema hayo jana katika sherehe za uzinduzi wa Jumuiya ya Kuzuia, Kukinga na Kuondosha Maafa na Majanga Zanzibar (DCPM), hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
Alisema kuwa Jumuiya na taasisi kama hiyo zinapaswa kuungwa mkono kwa dhati na kila mtu na kuihakikishia Jumuiya hiyo kuwa Serikali itashirikiana nayo kwa karibu sana.
Dk. Shein alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais inayo Idara ya kushughulikia maafa na majanga nchini hivyo ni vyema Jumuiya hiyo ikajenga uhusiano na ushirikiano mkubwa zaidi kwa apamoja ili kupata maarrifa ya ziada na kufanya kazi kwa pamoja.
Hivyo Dk. Shein alitoa wito kwa mashirika, taasisi na vyombo vyengine vifanye hivyo na pia Jumuiya hiyo izidi ushirikiano na taasisi zote zinazohusiana na masuala hayo hapa Tanzania na sehemu nyengine, ili kujiongezea maarifa na uwezo zaidi wa kiutendaji.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitilia mkazo mkubwa umuhimu wa elimu ya aina hiyo kusomeshwa kwa watoto skuli kama ilivyokuwa hapo miaka ya nyuma ambapo Polisi walikuwa wakitoa elimi ya kuepuka ajali na Kikosi cha Zimamoto walikuwa wakitoa elimu juu ya kuzuia moto.
Sambamba na hayo Serikali haitosita kuchukua hatua itakapozibaini asasi ambazo zinatafuta na kupata misaada ya kifedha na vifaa nchini na nje ya nchi lakizi kazi zao hazionekani na nyengine hazina hata afisi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya hiyo Najima Murtadha Jiga, alieleza kuwa Jumuiya hiyo imeanzishwa ikiwa na dira ya kujenga uwakilishi madhubuti, ambao utahakikisha uelewa na elimu kwa jamii, na kutoa msaada katika kukabiliana na masuala yote ya maafa na majanga hapa Zanzibar .
Alieleza kuwa wazo la kuanzishwa kwa DCPM, limetoka miongozi mwa wananchama Waanzilishi wa Jumuiya, baada ya utafiti wa kina na kutafakari juu ya suala zima la maafa na majanga hapa nchini.
Aidha, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Jumuiya hiyo tayari ina katiba yake wenyewe, kanuni za kuendeshea Jumuiya na mkakati wa kipindi cha miaka mitano ambapo kufanikiwa kwa yote hayo kumetokana na jitihada za Wajumbe wa Kamati Tendaji.
Alieleza kuwa baada ya kutafiti na kuona kuwa suala la maafa na majanga lina uwanja mpana kabisa, Jumuiya ya DCPM itahakikisha inatoa elimu tosha kwa jamii ili waweze kuelewa yale yanayosababisha maafa na majanga na athari zinazoweza kutokea na pia kutoa msaada katika kukabiliana na suala zima la maafa na majanga iwe ni ya kimaumbile ama ya kibinaadamu.
Jumuiya hiyoimeanzishwa tarehe 1.1.2011 na kusajiliwa rasmi tarehe 17.6.2011 kwa mujibu wa Sheria no. 6 ya Asasi za Kiraia ya mwaka 1995 kwa usajili no. 957. Viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar .