Dk. Shein ataka SUZA ibadilike kimaendeleo

Nembo ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA)

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Wajumbe wa Baraza na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), na kueleza kuna haja ya chombo hicho kubadilika kiutendaji kwa lengo la kukiendeleza na kukiimarisha chuo.

Dk. Shein aliyasema hayo jana alipofanya mazungumzo na viongozi hao katika Kampasi ya Vuga, mjini Unguja mara baada ya kutembelea jengo la Taasisi ya Elimu Endelevu pamoja na kupata maelezo mafupi ya jengo la Majestik.

Katika maelezo yake kwa viongozi hao wa (SUZA), Dk. Shein alieleza kuwa umefika wakati kwa uongozi wa chuo hicho kubadilika ili kuweza kukiimarisha na kukiendeleza zaidi chuo hicho ambacho kinatimiza miaka kumi hivi sasa.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na viongozi waanzilishi wa Chuo hicho sanjari na kupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kukiimarisha na kukiendeleza chuo hicho ili kiweze kupata siafa zaidi ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza suala zima la utafiti.

Alisema kuwa Chuo Kikuu cha SUZA ni kama vyuo vikuu vyengine, tofauti ni majengo tu hivyo kuna kila sababu ya kuongeza juhudi kwa mashirikiano ya pamoja katika kukiendeleza na kukikuza chuo hicho.

“Huwezi kufanya kazi kwa mazoea, kuna muhimu wa kubadilika, kwani dunia inabadilika hivyo nasi tubadilike na naamini kuwa SUZA itabadilishwa na wanaSUZA wenyewe”,alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa anamatumaini makubwa ya mabadiliko ya Chuo Kikuu hicho kutokana na mikakati na malengo yaliowekwa na kusisitiza kuwa kubadilika kuanze kwa uongozi na ndipo kuje kwa wafanyakazi wengine na wanafunzi wa chuo hicho.

Alieleza malengo na madhumuni pamoja na mipango yote iliyowekwa katika kukiendeleza na kukiimarisha Chuo Kikuu hicho yatafikiwa iwapo patakuwa na mashirikiano ya kutosha pamoja na kutimiza wajibu uliopo. Dk. Shein alisema kuwa juhudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali katika kuhakikisha Chuo hicho kinapata majengo yake mapya huko Tunguu.

Alisema kuwa Chuo Kikuu hicho kuwa na majengo yake kutasaidia kwa kiasi kikubwa ambapo eneo la chuo la hivi sasa litabaki ni la historia kwa kuanzishwa chuo hicho na kusisitiza haja ya kuendeleza na kuimarisha eneo jipya la Tunguu ambalo litakuwa na miundombinu yote mipya sanjari na kuanzisha vitivo vipya na kuimarisha vile vya awali.

Katika maelezo yake hayo Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa wale wote wanayoiunga mkono serikali katika ujenzi wa chuo hicho ambao unatarajiwa kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.

Dk. Shein alisisitiza kuwa huu ni wakati muwafaka wa kuleta maendelea Zanzibar kutokana na amani na utulivu mkubwa uliopo hivi sasa, hivyo mabadiliko ni suala la lazima ili kuweza kukuza sekta ya elimu na kukuza maendeleo nchini.

Pia, Dk. Shein pia, alisisitiza haja kwa uongozi wa chuo hicho kuwasikiliza wanafunzi ili kuweza kujua matatizo yao huku akieleza azma ya serikali ya kuwasaidia waalimu kila pale hali inaporuhusu.

Akieleza msimamo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Shein alieleza kuwa serikali ina msimamo wa kuimarisha sekta ya elimu na kueleza kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ikifananishwa na nchi nyengine za Afrika ndani ya miaka 48 ya uhuru wake.

Alieleza kuwa tayari kuna wakuu wa vyuo vikuu tofauti duniani pamoja na wakufunzi wakiwemo kutoka Uturuki, Sharja na sehemu nyengine wameahidi kuja Zanzibar kukitembelea Chuo Kikuu hicho, wakiwemo wale aliowaalika yeye kuja kufanya hivyo, hizo ni kutokana na juhudi zake za kukitangaza chuo hicho ndani na nje ya Zanzibar.

Nao uongozi wa chuo hicho ulitoa pongezi kwa Dk. Shein kutokana na ziara yake hiyo na kueleza kuwa tayari chuo hicho kimeweka mikakati na mipango kabambe ya kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika kukuza sekta ya elimu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kulipa kipaumbele suala zima la utafiti.

Kesho, Dk. Shein anatarajiwa kuzungumza na wafanyakazi, Wahadhiri wa Chuo hicho pamoja na Wajumbe wa Baraza na Menejimenti huko katika ukumbi wa mkutano wa Chuo hicho uliopo Kampasi ya Nkrumah