Dk. Shein ataadhalisha juu ya chakula

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba Ikulu-Zanzibar

USALAMA wa Chakula nchini na duniani kote ni suala linalohitaji uangalizi mkubwa ili kuhakikisha haitokei uhaba wa chakula na watu wote wanapata mahitaji yao ya kutosha wakati wote hapa nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Baraza la Biashara la Zazibar (ZBC), huko katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa katika mkutano huo wa sita kumepangwa zaidi kuzungumzia usalama wa chakula na lishe hapa Zanzibar na kusisitiza kuwa uhaba wa chakula husababisha njaa, maradhi na unaweza kuleta kuyumba kwa uchumi na kuondosha utulivu wa nchi.

Alisema kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi nyengine nyingi za Afrika na kwengineko hutegemea kuagiza vyakula vya ziada kutoka nchi za nje na uagiziaji huu huongeza kadri idadi ya watu inavyoongezeka.

Dk. Shein alisema kuwa mabadiliko ya matumizi ya chakula yanayotokea duniani hivi sasa hususan kwa chakula cha aina ya nafaka ambacho kinahitajiwa na watu wengi duniani yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Rais alitolea mfano kuwa hivi sasa nafaka zinatumika sana kwa matumizi ya viwanda na malisho ya wanyama ambapo pia, matumizi ya sukari nayo yameongezeka kutokana na matumizi makubwa ya viwanda.

“Tunapaswa kuwa na utaratibu mzuri wa kuzalisha, kuagiza, kutumia na kuhifadhi chakula hapa nchini ili tujiweke katika hali ya usalama”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa uchumi wa nchi ndio gurudumu la maisha na kusisitiza kuwa ustawi wa biashara unaofanywa unategemea hali ya uchumi na maendeleo ya jamii katika sekta zake zote, zikiwemo afya, elimu, barabara, maji na nyenginezo.

Dk. Shein alisema kuwa uimarishaji na ukuaji wa uchumi ni miongoni mwa malengo makuu ya Serikali anayoiongoza.

Alisema kuwa mikakati na mipango mingi ya kukuza uchumi imekuwa ikitayarishwa na serikali na ni jambo la kuridhih kwamba sekta binafsi mara nyingi inashirikishwa katika utayarishaji wa mipango hiyo ikiwemo utayarishaji wa MKUZA I na mapitio yake yalioleta MKUZA II.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa wafanyabiashara wanalo jukumu kubwa la kuwa mstari wa mbele katika kustawisha uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa sera iliyopo ya uwekezaji inakubalika ndani na nje ya nchi.

Dk. Shein katika hotuba yake hiyo ya ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili aliahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kuliendesha Baraza la Biashara na kustawisha ushirikiano wa sekta za binafsi na za umma.

Alieleza kuwa anaelewa kuwa ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma ni muhimu sana katika kuiendeleza Zanzibar na hatimae kuwaletea mafanikio wananchi.

Rais Dk. Shein aliwaeleza wajumbe hao kuwa wajumbe kutoka mashirika mbali mbali ya Marekani yanayohusiana na biashara na uwekezaji watahudhuria kwa lengo la kutoa nafasi ya uwekezaji nchini mwao na kuwataka wajumbe wa ZBC kuitumia nafasi hiyo.

Dk. Shein pia, alitoa pongezi zake za dhati kwa Mwenyekiti wa ZBC aliyepita, Rais Mstaafu Dk. Amani Abeid Karume na kueleza kuwa atakumbukwa kwa heshima kubwa kwa kulianzisha, kuliongoza na kuliendeleza Baraza hili la Biashara la Zanzibar (ZBC).

Mkutano huo wa Sita ni wa mwanzo katika Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao pia, ni mkutano wa mwanzo ambao Dk. Shein anakuwa Mwenyekiti wa mkutano huo katia Baraza hilo la Biashara la Zanzibar.

Mapema Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Mazrui, akimkaribisha Dk. Shein kutoa hotuba yake ya ufunguzi alisema kuwa uchumi wa nchi nyingi duniani hutegemea mchango wa sekta binafsi.

Alisema kuwa sekta binafsi inaweza kufanya mambo makubwa katika kuleta maendeleo na kuahidi kuwa sekta ya umma itaendelea kuweka mazingia mazuri kwa sekta binafsi.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Philimon Luhanjo alieleza kuwa kumekuwa na mashirikiano mazuri kati ya Baraza la Biashara la Zanzibar (ZBC) na Baraza la Biasahara la Taifa (TNBC).

Viongozi mbali mbli walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, Mawaziri, Makatibu na viongozi wengine SMZ na SMT pamoja na wajumbe wa Baraza hilo wakiwemo wafanyabiashara na waekezaji.