Dk. Shein asema SMZ itawatunza wazee wa Unguja na Pemba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuwaenzi na kuwatunza wazee wa Unguja na Pemba.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Sebleni mjini Unguja, katika nyumba za kulelea wazee wakati alipokuwa akizungumza na wazee wanaoishi katika nyumba hizo, zilizojengwa mara baada ya Mapinduzi ya nmwaka 1964.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa historia ya kuwatunza na kuwalea wazee ipo, hivyo ni jukumu la serikali kuendeleza hatua hiyo ili wazee nao waishi katika mazingira bora yenye amani, utulivu na starehe. Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inakwenda sambaamba na Sera za ASP na Chama Cha Mapinduzi pamoja na Ilani yake iliyoeleza kuwa itawatunza wazee wa Unguja na Pemba.

Dk. Shien alieleza kufurahishwa kwake na azma ya Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake na Watoto kwa azma yake ya kuukarabati ukumbi wa nyumba hizo za wazee kwa ajili ya kuutumia wazee hao pamoja na jiko lake huku ikiendelea na ujenzi wa nyumba ambayo iliungua na moto hapo mwaka jana.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuwatunza wazee huku ikiwa inazingatia malengo ya Kimataifa ya kuwatunza na kuwaenzi wazee.

Alieleza kuwa katika kuendeleza malengo ya kuwatunza na kuwaenzi wazee, serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha wazee hao wanaishi katika mazingira bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuwapatia huduma zote muhimu zikiwemo za afya katika eneo la nyumba hizo. Pia, alieleza kuwa kwa mwenendo ule ule wa azma ya Mapinduzi na viongozi wake wote waliopita serikali itahakikisha inawatunza wazee kwa kuwapatia usafiri wa uhakika wazee hao ili uweze kuwasaidia katika shughuli zao.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa katika kuhakikisha wazee hao wanaishi katika maisha yaliobora zaidi serikali itafanya juhudi za kuhakikisha wazee hao wanapata chakula cha uhakika ambacho kitakuwa ni mlo wa kutwa mara tatu kama ilivyokawaida ambapo utaandaliwa utaratibu maalum kwa wazee wa Unguja na Pemba ambao Waziri muhusika atauelezea hapo baadae muda utakapofika.

Na kueleza kuwa hatua hiyo itawasaidia sana wazeee hao kwani posho wanalopewa wataweza kutumia kwa matumizi mengineyo na kusisitiza kuwa wazee hawatakuwa na haja ya kupita kuhangaika.

“Serikali itafanya maamuzi ya kuwenzi na kuwatunza wazee na riski ya chakula cha kutwa isiwe tatizo kwa wazee wale wa Unguja na Pemba,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein pia, aliiagiza Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2015 nyumba zote zilizomo katika eneo hilo ziwe zimefanyiwa ukarabati na matengezo mazuri ya kuwafanya wazee hao waishi maisha bora zaidi. Katika maelezo yake hayo aliitaka Wizara hiyo kuweka kipambele chake katika ujenzi na ukarabati wa majengo ya nyumba hizo za wazee na kusisitiza kuwa azma ya malengo la Mapinduzi ipo pale pale juu ya kuwatunzana akuwaenzi wazee hapa nchini.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alipongeza juhudi za Jumuiya ya Wastaafu wa SMZ za kuchimba kisima katika eneo la nyumba hizo za wazee. Huku akieleza hatua zitakazochukuliwa katika kulitatua tatizo la umeme katika nyumba hizo.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kwa makusudi kuyashughulikia maisha ya wazee kwani inatambua umuhimu wa wazee hao huku akisisitiza kuwa tayari suala la ulinzi wa uhakika kutoka kikosi vya JKU kimeanza ulinzi kufuatia wizi wanaofanyiwa wazee hao katka nyumba hizo.

Pia, alipongeza Jumuiya ya Al-Yamin kwa kuunga mkono na kujitolea kulikarabati jengo moja miongoni wa majengo yaliopo eneo hilo na kulijenga msikiti na kuwaahidi wazee hao kuwa Serikali iko pamoja nao mchana na usiku, huku akieleza kuwa ujenzi wa ukuta nao utasaidia .

Mapema Waziri wa Wizara hiyo alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi zake za kuendeleza malengo ya Mapinduzi na Serikali yake ya kuwatunza wazee kwa kuweza kuwapelekea huduma muhimu karibu na makaazi yao ikiwa ni pamoja na ukarabati ya jengo, ujenzi wa ukuta pamoja na visima vya maji huku akieleza jinsi wazee hao walivyofurahia nyongeza ya posho lao.

Sambamba na hayo Waziri huyo aliwasilisha maombi matatu ya wazee hao likiwemo usafiri, Daktari wa kuwahudumia wazee hao wakati wote, usafiri na ulinzi ambayo yote hayo Dk. Shein aliyatolea ufumbuzi wake hapo hapo.