Dk Shein Asema Serikali Itapambana na Wavuruga Amani

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kulizindua Tawi la CCM Makombeni, akiwa katika ziara ya kuimarisha Chama katika Wilaya ya Mkoani Pemba leo,[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na wanamaskani ya Kidimni Jimbo la
Chamabani leo, akiwa katika ziara ya kuimarisha Chama katika Wilaya ya Mkoani Pemba leo,(kulia) Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai,[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]

Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Kusini Pemba, wakimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akizungumza nao leo katika ukumbi wa mikutano wa Skulimya Fidel kastro Vitongoji Chakechake  Pemba, akiwa katika ziara ya kuimarisha Chama katika  Mkoa wa Kusini  Pemba,[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]


Na Rajab Mkasaba, Pemba

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali haitomvumilia mtu/kundi lolote, litakalojiingiza kwenye siasa, kwa kutumia mrengo wa dini na kutishia kuvurugika kwa amani nchini.

Dk. Shein alieleza hayo, huko uwanja wa mpira Makombeni, mara baada ya kulifungua tawi la kisasa la CCM Makombeni, na baadae kuzungumza na WanaCCM na wananchi wengine, kwenye mkutano wa hadhara.

Alisema, katika siku za hivi karibuni, kumeibuka makundi yakitumia vibaya, fursa ya kutangaaza dini na kuchukua baadhi ya vipengele vya siasa na kuwababaisha wananchi, jambo ambalo halileti taswira nzuri katika taifa kama hili, lililotawala amani na utulivu.

Makamu Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa kamwe Serikali kwa kushirikiana na vyombo vyake, haitoyavumilia makundi hayo, kwani yamekuwa yakiitumia fursa hiyo vibaya. Alieleza kuwa ndani ya Serikali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa, hakuna sababu ya kurejeshana kule taifa lilikotoka, na badala yake ni vyema fursa za kujikusanya na kuhutubia zikawa zinahubiri umoja, amani na mshikamano.

“Kundi lolote likigundulika linatumia vibaya fursa ya kutangaza dini, na kujikita kwenye mambo ya kisiasa kwa lengo la kuwagawa wananchi na kuvuruga amani na utulivu uliopo halitovumiliwa,”alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, alieleza kuwa, Serikali inayoongozwa na CCM tayari imeanza mchakato wa kuifanya hospitali ya Abdallah Mzee ya Mkoani, kuwa ya Mkoa kama ilivyoahidiwa wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

“Wakati tulipokuwa tukipita katika kuomba ridhaa ya kuongoza nchi, tulisema kuwa mkituchagua tutafanya mengi, ikiwa ni pamoja na kuifanya hospitali hiyo kuwa ya Mkoa, sasa mambo yameanza katika kuitekeleza ahadi hiyo,” alifafanua.

Kuhusu dhana zilizoibuka hivi karibuni, kwamba vyama vya upinzani vitamuondoa Dk. Shein madarakani, kutokana na wingi wa kumiliki vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, hao alisema wamechelewa. Alieleza kuwa, yeye hawezi kung’olewa madarakani kwa wingi wa vitambulisho hivyo vinavyomilikiwa na wafuasi wa chama fulani, kwani kinachohesabiwa siku ya uchaguzi mkuu, ni kura na sio vitambulisho.

Alizidi kufafanua kuwa, wenye ndoto hizo wamechelewa na wamekuwa wakiota ndoto za mchana, ambazo hukosa jawabu makini na kubaki wakitapatapa. Akieleza kuhusu Katiba ya Zanzibar, alisema kila mmoja anawajibu wa kuifuata kwa vitendo, maana hakuna mtu wala kundi la watu lililojuu ya katiba ya nchi.

Katika hatua nyengine Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, aliwataka vijana, waache tabia ya kukimbilia nje ya nchi kwa kutafuta kazi, na badala yake watulie nchini ili kujikusanya pamoja kwenye vikundi vya ushirika.

Alifafanua kuwa, Serikali imekuwa mbioni kila siku kuhakikisha vijana wake wanawezeshwa kupitia vikundi vya ushirika, kwani Serikali haina uwezo wa kuajiri kila mmoja. Mapema Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar aliwakabidhi kadi za CCM wanachama wapya 291wakiwemo wa Jumuia za CCM, mara baada ya kulifungua tawi jipya la kisasa la CCM Makombeni.

Awali dk Shein na ujumbe wake, ulitembelea tawi la CCM la Mizingani na ambapo yeye mwenyewe peke yake aliahidi kuchangia shilingi milioni 2 ambapo viongozi wengie aliofuatana nao katika harambee iliyofanywa hapo hapo waliahidi kuchangia shilingi milioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa matawi ya kisasa ya CCM ya Mizingani na Chambani.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema tayari CCM imeshajipanga vyema kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chambani.

“Sisi CCM tunasema kuwa tuko tayari kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Chambani, na hatuendi kushiriki tunaenda kushindana,” alisema Vuai.

Hata hivyo, alisema CCM, itaendelea kushinda katika kila chaguzi zinazoandaliwa hapa nchini, kutokana na ubora na uimara wa sera zake kwa wananchi. Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba wakati akiwasilisha taarifa ya Mkoa ya kichama huko skuli ya sekondari ya Fidel Castro, alisema CCM imejipanga vyema katika kuimarisha idadi ya wanachama.