Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amekabidhiwa ripoti ya kuzama kwa Meli ya MV Skagit na Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo, na kuahidi atahakikisha mapendekezo yote yaliotolewa na tume hiyo yanafanyiwa kazi.
Mara baada ya kupokea ripoti, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Tume hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na kusema jitihada za makusudi zitachukuliwa na Serikali kuhakikisha mapendekezo yote yaliotolewa katika ripoti yanatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Alisema kufanikiwa kwa ripoti hiyo ambayo imechukua muda mfupi, kumetokana na uzoefu mkubwa wa wajumbe wa tume hiyo kwani wajumbe hao ndiyo waliochunguza kuzama kwa MV Spice Islander mwezi Septemba, 2012.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa taarifa zaidi zitatolewa kwa wananchi juu ya uchunguzi huo pamoja na hatua zitakazochukuliwa na serikali sambamba na kuiweka ripoti hiyo kwenye mtandao kwa lengo la kuwahabarisha wananchi.
Alisisitiza kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi na serikali kwa kuzingatia haki na uadilifu pamoja na kuzingatia sheria na taratibu za nchi zilizopo. Mapema Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Uchunguzi wa kuzama kwa Meli ya MV Skagit, Jaji Abdulhakim Ameir Issa alimueleza Dk. Shein kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi zake Agosti 1, 2012 na kumaliza Septemba 15, mwaka huu imefanya kazi vizuri baada ya kupata mashirikiano ya kutosha kutoka kwa wahusika.
Alisema kuwa Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 10, chini ya Jaji Abdulhakim Ameir Issa ilipita katika maeneo mbali mbali ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam wakati wakifanya shughuli zao hizo na kuweza kupata mafanikio. Mwenyekiti huyo alimueleza Rais sababu zilizopelekea kuzama kwa meli hiyo pamoja na mapendekezo ya Tume hiyo waliyoyapendekezwa.
Tume hiyo iliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein tarehe 23 Julai mwaka huu ambayo wajumbe wake ni Mwenyekiti Jali Abbdulhakim Ameir Issa, Katibu wake Shaaban Ramadhan Abdalla.
Wengine ni Salum Toufiq Ali, Kepteni Hatib Katandula, Bi Mkakili Fausta Mbowi, Komodoo Hassan Mussa Mzee, Meja Jenerali S.S. Omar, Kepteni Abdalla Yussuf Jumbe, Kepteni Juma Abdalla na Bwana Omar Chengo. Akitoa neon la shukurani kwa niaba ya Tume hiyo Bwana Omar Chengo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ni imani yao kubwa kuwa wamefanya kazi vizuri tena kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skagit ilitokea Julai 18 mwaka huu mnamo majira ya saa 7:30 za mchana, wakati meli hiyo ikitokea Dar-es-Salaam kuja Zanzibar ikiwa na abiria 447 pamoja na mizigo kadhaa. Ambapo alieleza kuwa katika ajali hiyo watu 212 wamepotea na watu 154 walinusurika na waliokufa walifikia idadi ya 81.