Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, leo ameongoza mazishi ya marehemu Mheshimiwa Salum Amour Mtondoo, aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo la Bububu, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Viongozi mbalimbali wa Vyama, Dini na Serikali wakiwa pamoja na wananchi na wanafamilia walihudhuria katika mazishi hayo, ambapo Makamu wa Kwanza wa Rais Alhaj Maalim Seif Sharif Hamad nae alihudhuria.
Alhaj Balozi Seif Ali Idd pamoja na Rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi nae alihudhuria katika mazishi hayo yaliofanyika saa nne asubuhi huko kijijini kwao marehemu Bumbwini Misufini, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo maiti aliondokea nyumbani kwake Bububu baada ya kusaliwa katika msikiti Utapoa Bububu.
Salum Amour Mtondoo alifariki dunia jana tarehe 15/3/2012 kwenye hospitali ya MnaziMmoja, ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu. Mtondoo alizaliwa tarehe 14/12/1962 Bububu, Wilaya ya Magharibi, Zanzibar na kupata elimu yake ya msingi na Sekondari katika Skuli ya Bububu kuanzia mwaka 1969 hadi 1979.
Akisoma risala fupi baada ya mazishi hayo, Kaimu Katibu wa Baraza la Wawakilishi Yahya Khamis alieleza kuwa katika shughuli za ajira rasmi, marehemu aliwahi kufanya kazi ya Usimamizi wa Kiwanda cha kutengenezea nguo cha COTEX kuanzia mwaka 1983 hadi mwaka 1985.
Alieleza kuwa nje ya ajira rasmi, marehemu alifanya kazi za Ujenzi katika Ushirika wa Bait-El-rs Building Brigade (BBB) hadi mwaka 1986 hadi mwaka 1992. Vile vile, aliwahai kufanya kazi za biashara kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 1020.
Katika shughuli za kisiasa, marehemu amewahi kushiriki nyazifa mbali mbali katika Chama Cha Mapinduzi zikiwemo Ujumbe wa Kamati ya Siasa ya Tawi na Ujumbe katika Jumuiya ya Wazazi Wilaya na Mkoa.
Salum alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Bububu katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Octoba, 2010 ambapo katika Baraza la Wawakilishi alikuwa mjumeb wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi na aliitumikia Kamati hiyo hadi muda wote wa Uwakilishi wake.
Katika kipindi cha kifupi cha kazi yake ya Uwakilishi, Marehemu alifanya kazi nzuri ya kuwatetea wananchi wa Jimbo lake pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, na aliifanya kazi hiyo kwa moyo wake wote, uadilifu na mashiruikiano makubwa kwa wananchi na Wajumbe wenziwe wa Baraza la Wawakilishi
Kaimu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa ni dhahiri kuwa Baraza la Wawakilishi, Chama Cha Mapinduzi, Wananchi wa Jimbo la Bubu na wananchi wote wa Zanzibar kwa jumla wameondokewa na mtu muhimu aliyesaidia katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Wengine waliotoa salamu zao kwa niaba ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar Vuai Ali Vuai ambaye alieleza kuwa kifo cha Marehemu Mtondoo kimeacha pengo kubwa katika CCM, ambapo alikiri kuwa Chama hicho kimeondokewa na mtu muhimu ambaye bado walikuwa wakimuhitaji na kuahidi kuwa Chama kipo pamoja nae.
Naye Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho akitoa salamu za Baraza la Wawakilishi alieleza kuwa marehemu Mtondoo alikuwa kiungo muhimu cha Baraza hilo kwani alikuwa akifanya kazi zake kwa umakini na mashirikiano ya makubwa.
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, akitoa salamu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisema kuwa Marehemu Mtondoo ameacha pengo kubwa ambalo si kwa wananchi wa Bububu pekee bali ni pengo kwa Zanzibar nzima na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iko pamoja na wafiwa.
Nao wanafamilia walitoa shukurani zao kwa viongozi wote pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wa Jimbo la Bububu kwa mashirikiano makubwa waliyoyapata katika kipindi chote cha msiba huo wa mwanafamilia yao. Marehemu ameacha vizuka watatu na watoto 10.