Dk Shein Aongoza Hitma ya Mzee Abeid Amani Karume

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na wakuu wa Vikosi vya ulinzi
alipowasili katika viwanja vya Ofisi ya CCM Kisdiwandui Mjini Unguja
kuhudhuria katika Hitma ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume, [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu.]

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj
Dk.Jakaya Mrisho Kikwete,akisalimiana na wakuu wa Vikosi vya ulinzi
alipowasili katika viwanja vya Ofisi ya CCM Kisdiwandui Mjini Unguja
kuhudhuria katika Hitma ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Wananchi na Waumini wa Dini ya Kiislamu wakisoma Hitma
Kumuombea Dua Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume,katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya CCm Kisiwandui Mjini
Zanzibar,ambapo kila ikifika siku kama hii wananchi kwa ujumla wao
hukusanyika kuomba dua kama hii, [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo pia, ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Kharib Bilal, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi pamoja na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

Kiongozi wa Kihindu akiomba dua wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa (Karume Day) katika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar leo April 7, 2013. (Picha na Ikulu)

Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mama Fatma
Karume,(kulia) akiwa na Wake wa Viongozi mbali mbali katika Hitma ya
Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume,huko
Ukumbi wa CCK Kisiwandui Mjini Zanzibar Leo, [Picha na Ramadhan
Othman,Ikulu.]


Viongozi wengine ambao walihudhuria katika hitma hiyo ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis
Haji, Sheikh Mussa Salum kutoka Mkoa wa Dar-es-Salaam naye alihudhuria pia.

Wengine ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi, wananchui kutoka sehemu mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin na kuongozwa na Sheikh Yussuf Mohammed Khamis. Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Mkoa wa Dar-es-Salaam, Sheikh Mussa Salum alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na kumuombea Mwenyezi Mungu ampe makaazi mema Peponi.

Akieleza kuhuhu umauti, Sheikh Mussa alisema kuwa umauti ni jambo ambalo litafika kwa kila kiumbe alichokiumba MwenyeziMungu nakusisitiza kuwa ni vizuri mwanaadamu akakumbuka asili yake na hatma yake.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui dua liyoongozwa na viongozi wa dini tofauti akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabhi, Askofu Michael Hafidh kutoka Kanisa la Anglikana Zanzibar.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri
Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Ramadhan Haji Faki aliyeweka shada la maua akiwakilisha wazee walioshiriki Mpinduzi ya Januari 12, 1964.

Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Hassan Vuai Chema, Balozi Ali Karume aliyewakilisha watoto wa Marehemu Karume na Balozi mdogo wa Misri anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi Walid Mohamed Ismail aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa hapa nchini na Ahmed Amani Karume aliyewakilisha wajukuu.

Aidha mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, alishiriki katika hitma hiyo akiongozana na Mama Salma Kikwete, Mama Asha Balozi na Mama Pili Balozi, Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 41 tokea utokee msiba huo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.