Dk Shein aongoza hitma ya Abeid Aman Karume

”]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo pia, ilihudhuriwa na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Kharib Bilal pamoja na Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume.

Wengine ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar. Hitma hiyo ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Rashid Jaffar na kuongozwa na Sheikh Mohammed Kasim kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Mussa Salum alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyewatetea wanyonge na aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Akieleza kuhuhu umauti, Sheikh Mussa alisema kuwa umauti ni suala la kubadilisha maisha mengine ambayo yanakizuizi na mazingira maalumm hivyo alisisitiza kuwa jambo kubwa kwa kila mmoja ni kuangalia amejiandaa vipi na umauti na pia ajue kuwa Allah ameumba uhai na umauti ili awajaribu viumbe wake na kusisitiza kuwa kila mmoja ajue huku akiwa na mazingatio kuwa ipo siku nae ataelekea katika safari hiyo ya umauti.
Viongozi wengine ambao pia, walihudhuria katika hitma hiyo ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Meja Jenerali Hassan Vuai Chema, muwakilishi wa familia ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere, Sheikh Mussa Salum kutoka Mkoa wa Dar-es-Salaam nae alihudhuria.
Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili, viongozi hao na wananchi walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui dua iliyoongozwa na viongozi wa dini mbali mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar akiwemo Mufti Mkuu Sheikh Kabhi, Sheikh Mussa Salum kutoka Dar-es-Salaam na Askofu Cosmas Shao kutoka Kanisa la Minara miwili Zanzibar.
Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Hassan Vuai Chema, Balozi Ali Karume na Balozi mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi Bernado Libimba aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa hapa nchini na Ahmed Karume aliyewakilisha wajukuu.
Aidha mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, alishiriki katika hitma hiyo akiongozana na Mama Asha Balozi na Mama Pili Balozi, Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.
April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 40 tokea utokee msiba huo.