Dk Shein amzika Kanali Magetta Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, (wa tatu kulia) pamoja na Viongozi wengine wakiusalia mwili wa Marehemu Kanal Nassor Waziri Magetta, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Valantia, katika msikiti masjid Twariq Bububu nje wa Mji wa Zanzibar, aliyefariki jana na kuzikwa Kijiji kwao Mkanyageni Wilaya ya Magharibi Unguja.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameungana na viongozi, wananchi na wanafamilia katika mazishi ya Marehemu Kanali Nassor Waziri Magetta eneo la Mkanyageni, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Katika mazishi hayo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, serikali wa viongozi wa kidini walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Marehemu Kanali Magetta amefariki dunia jana alfajiri nyumbani kwa mtoto wake Bububu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kanali Magetta ambaye amefariki akiwa katika Utumishi wa Idara Maalum Kikosi cha Valantia cha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amezaliwa mwaka 1938, katika kijiji kiitwacho Tawa, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Mkoa wa Morogoro Tanzania Bara.

Tokea utoto wake Marehemu Magetta aliishi Zanzibar katika kijiji cha Nduduke Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kupata elimu yake ya msingi katika skuli ya Dole na pia kupata elimu ya Korani.

Marehemu Magetta aliitumikia serikali ambapo alijiunga na Jeshi la Ukombozi la Zanzibar (JLU) Julai 1964 na baade kuendelea na kazi hiyo katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambapo aliistaafu akiwa katika cheo cha Luteni Kanali mwaka 1989.

Mwaka 2005 Marehemu Magetta aliteuliwa kuwa Mkuu wa Utawala wa Kikosi cha Valantia Zanzibar akiendelea akiwa na cheo cha Kanali Usu (Lt Col) ambapo mwaka mmoja baade alipandishwa cheo cha Kanali na kuteuliwa kuwa Mkuu wa KVZ Zanzibar cheo ambacho amefariki akiwa nacho.

Kwa upande wa kisiasa Marehemu Magetta wakati kilipoanzishwa chama cha Afro- Shirazi ASP mwaka 1957 alijiunga na kua mwanachama na ulipoundwa Umoja wa Vijana wa chama hicho pia hakuchelea kujiunga.

Akiwa mwanachama wa ASP na Umoja wa Vijana wa ASP, alikuwa miongonimwa viongozi wa ASPYL akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Vijana sanjari na kuwa wanachama mwanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi wakati kilipoanzishwa mwaka 1977. Marehemu ameacha kizuka mmoja na watoto watatu