Dk Shein amaliza ziara Kusini Pemba

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika Majumuisho ya Ziara aliyoifanya katika Mkoa huo, Ukumbi wa kituo cha chuo cha Amali Vitongoji. Picha na Ramadhan Othman, Pemba.

Na Rajab Mkasaba, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amemaliza ziara yake katika mikoa mitano ya Zanzibar na kueleza kuwa Serikali imeamua kuimarisha zao la karafuu ikiwa ni pamoja na kupandisha bei ya zao hilo ili kuwanufaisha wakulima.

Dk. Shein ameyasema hayo leo katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati akifanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo. Katika ziara hiyo Dk. Shein alifuatana na mkewe, Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa vyama na Serikali.

Akizungumza Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imechukua hatua za kuliendeleza zao la karafuu ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango maalumu ya kuliimarisha.

Alisema mipango ya kuliimarisha zao hilo itakwenda sambamba ikiwa ni pamoja na kupanda mikarafuu mipya, kuwaendeleza wakulima wake na kuwajengea mazingira mazuri ya bei.

“Serikali ina mpango wa makusudi kuweka bei nzuri ya karafuu itakayowavutia na kuwaletea wakulima tija zaidi,” alisema na kuwapongeza wakulima kwa jitihada zao za kuonesha nia ya kuliendeleza zao la karafuu. “Sisi tumejidhatiti kuimarisha kilimo ikiwemo zao la karafuu,” alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema katika kusimamia mapinduzi ya kilimo, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, imeielekeza SMZ kuliendeleza zao la karafuu.

Pamoja na hayo, Dk. Shein katika hotuba yake amesema Serikali imedhamiria kupambana na tatizo la wizi wa mifugo hasa ngombe na kusisitiza taratibu za kusafiisha mifugo, wanyama waliochinjwa na mazao ziimarishwe ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria zilizopo.

“Kama unataka kuchinja nyama ya ngombe kanunue wako, iweje umuibe ngombe wa mwenzio halafu umchiche…kamanda washughulikieni wezi hawa kwa taratibu za nchi zilizowekwa,” alisema Dk.Shein.

Dk. Shein pia, aliwataka viongozi wa mkoa huo kuhakikisha wanatoa taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa wao kwa wao.