Dk. Shein Akutana na Mabalozi wa Nchi za Canada na Cuba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Jorge Luis Lopes, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana. [Picha na
Ramadhan Othman, Ikulu]



Na Said Ameir, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana, kwa nyakati tofauti, alikutana na Mabalozi wa nchi za Canada na Cuba ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na nchi hizo.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Canada nchini Bwana Alexandre Leveque, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania inathamini na kujivunia uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya serikali na wananchi wa nchi mbili hizo.

Dk. Shein alisema uhusiano kati ya Tanzania na Canada umejengwa katika misingi ya usawa na kuheshimiana ambapo viongozi wa nchi hizo wamekuwa wakitembeleana mara kwa mara pamoja na kushirikiana katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwa ni njia mojawapo za kuimarisha uhusiano huo.

Dk. Shein alibainisha kuwa chini ya ushirikiano huo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikichangia katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]


Alizitaja Dira za Maendeleo ya 2020 kwa Zanzibar na 2025 kwa Tanzania Bara pamoja na Mikakati ya kuondoa umasikini nchini MKUZA kwa Zanzibar na MKUKUTA kwa Tanzania Bara kuwa miongoni mwa programu za maendeleo ambazo Canada imekuwa ikiziungwa mkono. Alizitaja sekta nyingine kuwa ni elimu, afya na uimarishaji wa utawala bora.

Kwa hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali na wananchi wa Canada kwa misaada hiyo ambayo aliieleza kuwa imesaidia kuharakisha jitihada za Serikali na wananchi wa Tanzania kujiletea maendeleo.

Katika mnasaba huo Dk. Shein alimuhakikishia Balozi wa Canada nchini juu ya dhamira ya dhati iliyonayo Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha ushirikiano uliopo na kupanua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ikiwemo uwekezaji katika sekta ya utalii Zanzibar.

Kwa upande wake Balozi wa Canada nchini Bwana Alexandre Leveque alieleza kufarijika kwake kwa kupata fursa ya kuitumikia nchi yake nchini Tanzania nchi ambayo aliieleza kuwa imekuwa na uhusiano mzuri na wa kihistoria. Uhusiano huo mzuri alieleza kuwa umetoa fursa na kuweka mazingira mazuri kwa nchi yake kuchangia jitihada za Serikali na wananchi wa Tanzania za kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii.

Alisema jukumu lake kubwa akiwa nchini ni kuhakikisha kuwa uhusiano huo unaimarika na kufungua milango katika maeneo mapya ya ushirikiano hasa katika sekta ya uwekezaji katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi wa Tanzania na Cuba ni wajibu kwa kuwa uhusiano huo ulioasisiwa na viongozi wa kwanza wa nchi hizo sio tu ni wa kihistoria bali ni wa udugu usiovunjika.

Akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Bwana Jorge Luis Lopes Tormo Ofisini kwake Ikulu mjini Zanzibar jana Dk Shein alisema kitendo cha serikali ya Cuba kuwa nchi ya kwanza kutambua mapinduzi matukufu ya Zanzibar mara yalipofanyika Januari 1964 ni kielelezo kuwa nchi hiyo na wananchi wake ni rafiki wa kweli.

Kwa hiyo amemhakikishia Balozi wa Cuba nchini kuwa serikali na wananchi wa Tanzania wataendelea kuiunga mkono Serikali na wananchi wa Cuba katika kulinda uhuru, heshma na maslahi ya nchi yao ikiwemo kupinga jaribio lolote la kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi. Dk. Shein aliishukuru Serikali ya Cuba kwa misaada yake ikiwemo kutoa fursa za mafunzo kwa vijana wa kitanzania wakiwemo wa Zanzibar katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya.

Alifafanua kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba umewezesha Zanzibar kupata misaada ya kiufundi katika sekta ya elimu na afya ambapo kwa miaka mingi Cuba imekuwa ikitoa walimu kufundisha pamoja na madaktari kufanya kazi Zanzibar.

Naye Balozi Tormo aliishukuru Serikali na wananchi wa Tanzania kwa kupinga azimio la kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi yake kitendo ambacho kilizuia maafa na madhila ambayo wangeyapata wananchi wa Cuba kama vikwazo hivyo vingepitishwa. Balozi Tormo alieleza kuwa ushirikiano wa watu watu wa Cuba na Zanzibar ulioanza tangu enzi za vuguvugu la kimapinduzi umekuwa wa faida kwa serikali na wananchi wa nchi mbili hizo. Aliongeza kuwa Cuba itauenzi uhusuano wake na Tanzania na nchi yake itahakikisha uhusiano huo unakuwa na kuimarishwa siku hadi siku kwa manufaa ya serikali na wananchi wa Cuba na Tanzania.