DK Shein Akutana na Kamati ya Mapinduzi CUP

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na Kamati ya mashindano ya ‘Mapinduzi Cup’ na kupongeza juhudi walizozichukua katika kufanikisha mashindano hayo yaliyoyafanyika katika kusherehekea miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamati hiyo chini ya mlezi wake, Balozi Seif Ali Idd pamoja na Wahisani waliochangia mashindano hayo ambapo pia, uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) nao ulikuwepo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Kamati hiyo kwa kuendeleza mashindano hayo ambayo yamefana kwa kiasi kikubwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mohammed Raza ambaye pia, ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini.
Dk. Shein mbali ya pongezi kwa kufanikiwa kwa mashindano hayo pia, alitoa pongezi kwa timu ya ‘Azam FC’kwa kupata ushindi kwa mara ya pili wa mashindano hayo na kupelekea kombe kubakia katika udongo wa Tanzania.
Alisema kuwa ushindi huo umeipa heshima kubwa Tanzania na kusisitiza kuwa michezo hujenga mshikamano, udugu na maelewano makubwa miongoni mwa jamii kwani ni sehemu ya maisha.
Dk. Shein alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika Kamati hiyo kutokana na uaminifu mkubwa ulioonesha wakati wa matayarisho ya mashindano kupitia kwa wahisani ambao walimeonesha moyo mkub wa wa kuyasaidia mashindano hayo pamoja na kuisaidia nchi hiyo.
Alieleza kuwa hatua kama hiyo inaweza kusaidia katika kuendeleza mambo mbali mbali ikiachiliwa mbali mashinadno ya mpira lakini kubwa kuliko yote ni uaminifu.Katika maelezo yake hayo, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika michezo mbali mbali hasa mpira wa miguu hivyo kuna haja ya kujiandaa vizuri zaidi katika mashindano hayo hapo mwakani ambapo sherehe za Mapinduzi zinatimiza nusu karne.
Aliunga mkono rai ya Kamati hiyo kupitia Balozi Seif kwa azma yake ya kukutana na Ubalozi wa China kwa lengo la kuialika timu kutoka nchini humo na yeye akasisitiza iwapo kuna haja ya kuyanogesha zaidi mashindano hayo naye yuko tayari kuialika Vietnam nayo kuleta timu yake kwani tayari Zanzibar imeshajenga uhusiano mwema na nchi hiyo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya kujiandaa katika mashindano hayo kitimu kwa kutoa mialiko sehemu mbali mbali zikiwemo ndani na nje ya Bara la Afrika pia, ni vizuri Kamati hiyo kwa kushirikiana na ZFA ikaangalia uwezekano wa kuweka nyasi bandia katika uwanja wa Aman mjini Unguja ili uweze kuchezeka vizuri.
Alisema kuwa Serikali iko tayari kuiunga mkono Kamati hiyo ili kufanikisha azma yake hiyo huku akisisitiza kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kurudisha heshima yake katika michezo hasa mpira wa miguu kwani Zanzibar ina historia katika medani ya soka.
Nae Balozi Seif Idd, alitoa pongezi zake kwa Kamati hiyo na uongozi wake na kueleza kuwa mashindano hayo yamekuwa kivutio cha watazamaji wengi na kupelekea kunogesha sherehe hizo na kueleza haja kwa Kamati hiyo kuwa Washajihishaji wa michezo hapa Zanzibar.
Balozi Seif alisema kuwa mikakati maalum imewekwa katika kuhakikisha mashindano yajayo hapo mwakani yanakuwa ya aina yake kwa kuzishirikisha timu nyingi huku akieleza nia yake ya kuzungumza na Balozi wa China ili kuleta timu kutoka nchini humo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk nae alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa azma yake ya kuimarisha michezo huku akisisitiza kuwa busara za Rais ndizo zilizoleta mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kuipa fursa Kamati hiyo ili iendelee kufanya kazi za kuandaa mashinadano hayo.
Waziri Mbarouk, alimuhakikishia Dk. Shein kwamba Wizara yake, imo katika juhudi za kuhakikisha migogoro ndani ya ZFA inapatiwa ufumbuzi ili soka la Zanzibar lizidi kuimarika.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mohammed Raza alimueleza Dk. Shein kuwa Kamati hiyo imefanya kazi kwa mashirikiano makubwa huku akimueleza jinsi ilivyojipanga katika mashindano hayo hapo mwakani kwa kualika timu kutoka sehemu mbali mbali zikiwemo za Afrika Mashariki na Kati, Afrika Magharibi na kwengineko.
Mhe. Raza alieleza jinsi wahisani waliochangia mashindano hayo walivyuoonesha moyo wao mkubwa katika kutoa michango yao huku akimueleza Rais kuwa Kamati hiyo haina deni hata moja kutokana na mashindano hayo pamoja na kueleza jinsi Kamati inavyofikiria kutafuta waamuzi kutoka nje ya nchi katika mashindano yajayo.
Katika hafla hiyo pia, Dk. Shein aliwakabidhi vyeti maalum wahisani waliofanikisha mashindano hayo wakiwemo Shirika la Bandari Zanzibar, Benki ya Watu wa Zanzibar, Hassan & Sons, Royal Furniture and Décor Ltd, Zanzibar Ocean Views Ltd, Zanzibar Aviation Services (ZAT), United Petroleum Ltd, Zan Air Ldt.
Wahisani wengine ni Pemba Misali Beach Resort na Zanzibar Insurance Corporation. Pia, Dk. Shein alimkabidhi tunzo maalum iliyoandaliwa na Kamati hiyo Rais wa ZFA. Bwana AmaniIbrahim Makungu kwa mchango wake mkubwa katika mashindano hayo.
Kwa maelezo ya Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Bi Sharifa Khamis Salim alizitaja timu nane ambazo zilishiriki katika mashindano hayo ambayo hatimae timu ya ‘Azam FC’ kuibuka kuwa mshindi ni pamoja na Tusker kutoka Kenya, Mtibwa, Simba, Jamhuri, Miembeni,Coastal Union, Bandari ya Zanzibar ambapo timu ya Yanga ya Dar-es-Salaam na Al, Ahly ya Misri zilijitoa.