Dk. Shein akabidhiwa ripoti ya uchunguzi Mv. Spice Islander

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, jana amekabidhiwa ripoti ya kuzama kwa Meli ya MV. Spice Islander na Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Abdulhakim Ameir Issa.

Mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Tume hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na hatimae kuandaa ripoti iliyoeleza juu ya tukio hilo. Dk. Shein aliipongeza Tume hiyo kwa jitihada kubwa ilizozifanya katika kuhakikisha uchunguzi wa tukio hilo unakamilika na hatimae kukabidhi ripoti.

Alieleza kuwa ripoti hiyo ni muhimu kutokana na tukio kubwa lililotokea na kuihakikishia Tume hiyo kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi.

Aidha, Dk. Shein aliahidi kuwa taarifa zaidi zitatolewa kwa wananchi juu ya uchunguzi huo pamoja na hatua zitakazochukuliwa na serikali. Mapema Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Uchunguzi wa kuzama kwa Meli ya MV Spice Islander Jaji Abdulhakim Amer Issa alimueleza Dk. Shein kuwa Tume imeridhika na uchunguzi uliofanya.

Aidha, Mwenyekiti huyo alitoa pongezi kwa mashirikiano mazuri iliyopata Tume yake katika kipindi chote cha Uchunguzi katika maeneo yote waliyopita pamoja na watu na watendaji wote waliokutana nao.

Dk. Shein aliunda Tume hiyo mwezi Septemba mara baada ya tukio la kuzama kwa meli ya MV Spice Islander ili kujua ukweli kuhusu chanzo cha ajali hiyo.