Dk Shein aipa changamoto Wizara ya Miundombinu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akiwa ziarani Pemba

Na Rajab Mkasaba, Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kuboresha kiwango cha utaalamu wa kujenga barabara kwa kutumia lami baridi, ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia hiyo mpya kusaidia ujenzi wa barabara kubwa za Unguja na Pemba.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ziara yake ya kuzitembelea barabara za Mizingani–Wambaa na barabara ya Chanjamjawiri-Tundauwa ikiwa ni miongoni mwa barabara sita za kisiwani Pemba zinazojengwa kwa kutumia utaalamu wa kutumia lami baridi ambao huwashirikisha wananchi wanaoishi karibu na pembezoni mwa barabara hizo zinazojengwa.
Akizungumza, Dk. Shein alisema utaalamu unaotumika katika kujenga barabara hizo maalum umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kupanua miundombinu ya mawasiliano ya barabara kisiwani Pemba hivyo kuna haja ya ujuzi huo kukuzwa zaidi ili uweze kutumika katika ujenzi wa barabara nyenginezo.

Dk. Shein ambaye alianza ziara yake ya kukagua barabara hizo hapo jana jioni ambapo alikagua barabara ya iyendayo Chanjani-Mitamani-Pujini na kusisitiza haja kwa Wizara husika kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya barabara kwa lengo la kuepuka ajali.

Akiendelea na ziara yake ya kuangalia mradi wa ujenzi wa barabara endelea leo na ziara hiyo alipongeza juhudi zilizochukuliwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasialno katika ujenzi huo na kutoa shukurani kwa wananchi wanaojenga barabara hizo. Katika mradi huo wa ujenzi wa barabara hizo wananchi hushirikishwa kwa kiasi kikubwa kwa kuweza kupata ajira na kuwa wasimamizi wa barabara hizo chini ya wataalamu na Makandarasi wengine.

Akisalimiana na wafanyakazi wa ujenzi wa barabara wakati alipotembelea barabara ya Chanjamjawiri-Tundauwa Dk. Shein aliwaeleza kuwa uwamuzi wao huo wa kushiriki katika ujenzi huo wa barabara ni jambo la busara na kuwapongeza kwa juhudi zao huku akiwaeleza jinsi Wizara husika itakavyoangalia namna ya kuwaendeleza.

Naye Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Mhe. Hamad Masoud alimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi wa barabara hizo uko katika hatua za mwisho ambapo kabla ya sherehe za Mapinduzi barabara zote sita zitakuwa tayari zimemaliza ujenzi wake.

Waziri huyo amemueleza Dk. Shein kuwa kuendelea kwa ujenzi huo kumepelekea wataalamu wengi wa ujenzi wa barabara kutoka maeneo na nchi mbali mbali za Afrika kufika kisiwani Pemba kwa ajili ya kupata utaalamu wa ujenzi wa barabara kwa kutumia teknolojia hiyo mpya kwemo Kenya, Msumbiji, Tanzania Bara na nchi nyenginezo.

Katika maelezo yake Waziri huyo wa Mindombinu na Mawasiliano alieleza kuwa tayari barabara tano zimeshakamilika na iliyobaki n hiyo ya chanjamjawiri-Tundauwa ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili zijazo. Pamoja na hayo, Waziri Masoud alieleza kuwa lengo la Wizara yake hiyo ni kuanzisha Wakala wa Barabara kama ilivyo kwa maeneo mengine ili barabara ziweze kujiendesha wenyewe kwa mambo madogo madogo.

Pamoja na hayo, uongoi huo wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ulimueleza Dk. Shein kuwa ujuzi na utaalamu huo uliotumika katika kujenga baadhi ya barabara kisiwani Pemba ambazo zilikuwa zikleta usumbufu mkubwa kwa wananchi hapo kabla pia, ujenzi huo utafanywa Unguja katika baadhi ya barabara mbali mbali. Walieleza kuwa miongni mwa Wakandarasi wanaosimamia barabara hizo wao kutoka Unguja na Pemba ambao wamekuwa wakishirikiana katika ujenzi wa barabara hizo na kusisitiza kuwa vifaa vya ujenzi vipo vya kutosha.

Nao wananchi wa maeneo zilimopita barabara hizo walitoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya Mapiduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa juhudi kubwa ilizochukua katika kuwajengea barabara hizo na kueleza kufurahishwa kwao na juhudi hizo.

Walieleza kuwa barabara hizo kwa hivi sasa zimewez kuwasaidia kwa kiasi kkubwa katika kuendeleza shughuli zao mbali mbali za maendeleo ikiwemo biashara, kilimo, uvuvi, uwekezaji na nyenginezo sanjari na kukuza na kurahisisha upataji wa huduma za kijamii. Wananchi hao walieleza kuwa kabla ya ujenzi wa barabara hizo changamoto mbali mbali zilikuwa zikiwakabili ambazo kwa hivi sasa ni historia.

Miongoni mwa barabara hizo zinazojengwa kwa kutumia teknolojia mpya ni Mtambile-Kengeja-Mwambe yenye urefu wa kilomita 9.4, barabara ya Mtambile-Kangani yenye urefu wa kilomita 6.5, barabara ya Mizingani-Wambaa yenye urefu wa kilomita 9.7, barabara ya Kenya –Chambani yenye urefu wa kilomita 3.2 na Chanjamjawiri-Tundauwa yenye urefu wa kilomita 11.

Zaidi ya Dola za Kimarekani 11.4 milioni zimetumika katika ujenzi wa barabara hizo chini ya ufadhili wa Serikali ya Norway kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Dk. Shein pia, katika ziara yake hiyo alitembelea maghala ya kuhifadhia karafuu huko katika Bandari ya Mkoani na kupata maelezo juu ya uendelezaji na uwekaji wa karafuu katika maghala hayo kwa ajili ya kusafirishwa bidhaa hizo kuletwa Unguja na hatimae kupelekwa nje ya nchi.