Dk. Shein ahaidi neema 2012 kwa Wazanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwaka 2012 imeahidi kuimarisha miundombinu na ubora wa huduma za jamii zikiwemo elimu, afya na maji safi na salama ili kwa pamoja visaidie kufikia lengo la kukuza uchumi na kupunguza umasikini, bila ya kuisahau dhamira kuu ya Mapinduzi ya Kilimo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar, katika risala aliyoitoa ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2012, AD na mwaka 1433 AH kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa jumla. Katika risala yake hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika mwa 2012, Serikali itaongeza ushirikiano na sekta binafsi katika kuchangia ukuaji wa uchumi na huduma za jamii.

Alieleza kuwa katika kukabiliana na athari za uchumi wa dunia hususan ongezeko la bei ya chakula, Serikali imejidhatiti kukabiliana na tatizo hilo kwa kuimarisha sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima. Akieleza mipango ya kiuchumi kwa mwaka 2012 Dk. Shein alisema kuwa Serikali inaazimia kuzidi kuongeza ukusanyaji wa kodi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Serikali yenu inapanga mipango bora zaidi ya kuiendeleza sekta ya Utalii ili kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anafaidika na sekta hii, huku tukiwa makini juu ya athari zake, na kwa hivyo kuulinda utamaduni, mila na silka zetu”alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa mazingira ya Utumishi bora katika kuwatumikia wananchi yatazidi kuimarishwa ili iwe chachu ya maendeleo ya haraka na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Alieleza kuwa masuala mengine yanayopaswa kukubushwa na kuyazingatia ni matukio makubwa ya Kitaifa likiwemo mchakato wa Katiba mpya ambapo ushiriki wa kila mmoja unahitajika na kuwanasihi wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni yao wakati utakapofika.

Aidha, alieleza jambo jengine la pili ni Sensa ya Taifa ya Watu na Makaazi, ambalo nalo ni tukio muhimu nchini kwani inapojulikana idadi ya watu ndipo upangaji bora wa huduma za uchumi na jamii unavyofanyika kwa ufanisi.

Kutokana na umuhimu huo wa Sensa, alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano katika zoezi hilo muhimu na kuwataka kuondoa hofu katika kujibu maswali watakayoulizwa na maafisa wa Sensa katika zoezi hilo litakalofanyika Agosti 26, 2012.

Dk. Shein alisisitiza kuwa katika kuelekea mwaka 2012 kuna mambo muhimu ya kuyazingatia na kuyatekeleza ipasavyo kwa ustawi wa maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha amani na utulivu. Jambo jengine ambalo Dk. Shein alilitaja ni kuongeza jitihada katika kukabiliana na vitendo vinavyosababisha uharibifu wa mazingira na kushusha hadhi na haiba ya mji.

Kutokana na hali hiyo Dk. Shein aliwataka wananchi wote kushirikiana na viongozi, taasisi za serikali na zisizo za Kiserikali katika kuondoa taka, kuzuwia uchimbaji ovyo wa mchana, uzururaji wa wanayama mijini na kuimarisha upandaji miti. Pia, alisisitiza kuondoa kabisa vitendo vya uzalilishaji wa kijinsia hasa ubakaji na kueleza kuwa tatizo hilo linafedhehesha sana na ni kinyume cha maadili ya Kizanzibari.

Sambamba na hayo, alisema kuwa licha ya kuwepo changamoto mbali mbali katika ukuaji wa uchumi nchini na kupanda kwa bei ya bidhaa duniani mafanikio makubwa yamepatikana katika ujenzi wa shule maalum za Sekondari za Wilaya Unguja na Pemba ambazo zimejengwa kwa kipindi cha mwaka mmoja badala ya miaka mitano.

Pia, alisema kuwa serikali imekamilisha ujenzi wa barabara kadhaa Unguja na Pemba pamoja na kuwapatia pembejeo za kilimo, mbolea, dawa na huduma za mashambani wakulima kwa bei nafuu zaidi. Dk. Shein alisema kuwa huu ni wakati wa kutafakari matukio ya mwaka unaomalizika na kasha kupanga mikakati ya kuimarisha mafanikio yaliopatikana na kuibua mbinu mpya za kukabiliana na changamoto zilizopo.

“Tutajifunza kuwa papo kwa papo kamba hukata jiwe, hivyo tunapaswa kujipanga upya ili tufanye vizuri zaidi mwaka unaokuja,” alisisitiza Dk. Shein.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa wakulima wa karafuu kwa kuziuza katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa (ZST) pamoja na kutoa pongezi kwa Kikosi Kazi kinachosimamia karafuu chini ya uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Wakuu wa Mikoa na Makamanda wa vikosi vya SMZ na SMT. Pia, alieleza imani yake kuwa kasi ya mabadiliko ya maendeleo itakuwa maradufu katika mwaka mpya wa 2012.