Na Rajab Mkasaba, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameendelea kuwafariji wafiwa kisiwani Pemba kufuatia ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv. Spice Islander na kueleza kuwa serikali itayafanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa na Tume hiyo juu ya ajali iliyotokea.
Dk. Shein, alieleza hayo kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akiwafariji wafiwa huko katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambako alikutana na wananchi katika maeneo maalum yaliyowekwa yakiwemo Skuli ya Wingwi, ukumbi wa Skuli ya Micheweni, Tumbe, Konde na Kinyasini
Dk. Shein alieleza kuwa taarifa hizo pia zitatolewa kwa wananchi ili nao wajue juhudi zilizochukuliwa na serikali yao. Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein amefuatana na Mama Mwanamwema Shein pamoja na viongozi wengine wakiwemo Mawaziri, Manaibu Waziri, Wabunge, Wawakilishi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na Kaskazini Unguja, wazee wa CCM pamoja na viongozi wengineo vyama na serikali.
Dk. Shein alisema kuwa Tume hiyo ya watu 10 aliyoiunda ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar pia, imejumuisha wataalamu kadhaa wa Sheria, manahodha waliobobea ambao wamefanya kazi kwa siku nyingi ndani na nje ya Tanzania, pamoja na wataalamu wengineo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mapendekezo yatakayotolewa na Tume hiyo yatafanyiwa kazi sambamba na yale yaliotolewa na Baraza la Usalama la Taifa. Dk. Shein alisema kuwa nia ya kutafuta meli nyengine kubwa ambayo itajumuisha safari kati ya Unguja na Pemba, Tanga na hadi Mombasa ipo huku juhudi zikichukuliwa za kuwashajiisha wafanyabiashara kuagiza meli hizo kubwa ambao baadhi yao wameonesha nia hiyo.
Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo ndio maana serikali haijalivunja Shirika lake la Meli la Zanzibar licha ya kutoa nafasi kwa biashara huru kwa kuweza kuwaruhusu watu binafsi kutoa huduma hiyo kwa wananchi.
Dk. Shein alisema kuwa madhumun ya ziara hiyo ni kutoa mkono wa pole na kuwafariji wafiwa pamoja na kuwapa pole wale wote waliopata majeraha na kuahidi kuwa serikali chini ya uongozi wake iko pamoja nao wakati wote.
Aidha aliwataka wale wananchi wote walioudhuria katika mikutano yake hiyo katika ziara yake kumtolea salamu zake za pole na ambirambi kwa wale walioshindwa kuhudhuria kwa sababu mbali mbali. Aliendelea kutoa shukurani kwa wananhi wote wa Unaguja na Pemba kwa umoja, mshikamano na mapenzi makubwa waliyoonesha katika kipindi chote cha msiba huo.
Dk. Shein alisema kuwa msiba huo ni wa wato wote, ni wa Waanzibar an Watanzania wote kwa jumla kwani wote umewagusa na kubwa lilobaki ni kuwa karibu na MwenyeziMungu na kuwaombea dua waliopata msiba huo na wale waliopoteza roho zao.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa mbali ya kutekeleza mapendekezo ya Tume hiyo pamoja na Baraza la Usalama pia, serikali im katika mikakati ya kujiandaa kimazingira ili kuepuka ajali kama hiyo kutotokea tena pamoja na kuepuka maafa mengineyo kutotokezea tena kwa rehema za MwenyeziMungu.
Alieleza kuwa serikali itafanya juhudi zake zote katika kusimamia safari za wananchi wao kutoka sehemu moja kwenda nyengine kwa kutambua kuwa maisha ya wananchi yanakuwa salama.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa salamu za pole bado inaendelea kutolewa kutoka nchi mbali mbali duniani pamoja na Taasisi na Mashairika ya Kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa ambapo Katibu Mkuu wake Ban Ki-Moon pamona na Naibu wake Dk. Asha -Rose Migiro pamoja na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso na wengineo.
Nao wananchi wa maeneo hayo katika Moa wa Kaskaini Pemba walitoa pongee na shukuran kwa Dk. Shein kufuatia ziara yake hiyo ya kuwafariji wafiwa na kueleza kuwa hiyo yote ni mitihani ya MwenyeziMungu kwani viumbe wote hatimae watarejea kwake.