Dk Shein aahidi neema kwa wavuvi Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akizindua Jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Weni-Wete.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wavuvi kufuata taratibu na sheria za uvuvi, wakati Serikali ikijipanga kuwawekea mazingira mazuri ya uvuvi kwa lengo la kufaidi kuelekea sherehe za Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Dk. Shein amesema hayo leo katika ufunguzi a jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Weni-Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 48 ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa iwapo wavuvi watafuata taratibu na sheria za uvuvi ili samaki wasitoweke pamoja na mazalio mengine ya baharini mafanikio makubwa yatapatikana.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi kwa upande wake ina mpango wa kuangalia upya sheria iliopo kwani inaonesha kuwa haiwabani sana wanaoivunja na badala yake hupelekea uvuvi haramu ushamiri sanjari na uharibifu mkubwa wa mazingira ya bahari.

“Wengine wanavua kwa kutumia vyandarua jambo hili ni hatari kubwa hivyo kuna kila sababu ya kuzingatia taratibu na sheria ziliopo,” alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza ufanisi wa shughuli za kazi za uvuvi na ufugaji katika kisiwa cha Pemba. Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo pia ni kupanua wigo katika kuwapelekea maendeleo wananchi ikiwa ni pamoja na kuendeleza maendeleo kutokana na Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964, ambayo yalimkomboa Mzanzibari na kumjengea heshima kutokana na madhila na mateso ya kutawaliwa.

“Elimu, afya, ardhi na menhgineyo ni mambo muhimu sana na ya msingi ambayo yamebainishwa katika Mapinduzi hivyo kuna haja ya kuyatilia mkazo na kuyafanyia kazi”,alisema Dk. Shein.

Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo pia ni miongoni mwa ahdi alizokuwa akizitoa wakati akikinadi Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu ulipita kuwa pindipo chama hicho kikishinda ataimarisha shughuli za ufuvi na ufugaji sanjari na kuwawekea mazingira bora wavuvi.

Alisema kuwa mbali ya hayo aliahidi kuwawekea mazingira boraya uvuvi na ufugaji vijana ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo juu ya shughuli hizo ndani na nje ya nchi ambapo tayari hivi karibuni vijana 30 kutoka Unguja na Pemba walikwenda China kwa ajili ya mafunzo hayo ambapo na mwaka huu pia wanatarajiwa kwenda wengine.

Pamoja na hayo Dk. Shein alieleza kuwa shughuli za uvuvi ni miongoni mwa shughuli za asili za watu wa Zanzibar ambapo kutokana na umuhimu wake katika uchumi wa wananchi na serikali kwa jumla, Serikali imeamua kwa makusudi kuziendeleza shughuli hizo ili ziwe na tija zaidi na endelevu.

Dk. Shein, aliwataka wavuvi hasa wale wanaokaa dago kuendelea kuhamasishana kutokana na maambukizi ya ukimwi huku akiahidi kuwashajiisha wafanyabiashara wanaonunua mwani kwa wakulima kuongeza bei ya zao hilo ili wawasaidie na waipende shughuli hiyo

Dk. Shein alitoa shukurani kwa Benki ya Dunia kwa kuendelea kuiunga mkono Zazibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ambapo pia, alieleza kuwa hivi karibuni aliziwekea mawe ya msingi skuli mpya za Sekondari Unguja na Pemba ambazo nazo zinatokana na mkopo wa benki hiyo.

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein pia, alisisitiza kuwa serikali imeweka mikakati maalum na mandalizi katika kuimarisha uvuvi hasa uvuvi wa bahari kuu ambao ni uvuvi wenye tija na unaohitaji vifaa na vyombo vikubwa vya baharini zikiwemo meli na boti za kisasa.

Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kwa Wizara hiyo na kutoa pongezi kwa uongozi pamoja na wafanyakazi wake wote kwa juhudi kubwa walizozichukua ndani ya mwaka mmoja na kupongeza kiasi cha fedha kilichchangiwa serikali na wizara hiyo ambazo ni asilimia 6 ya bajeti ya serikali kutokana na uvuvi.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Said Ali Mbarouk, alieleza kuwa sekta ya uvuvi iwapo itaendelea kutiliwa mkazo italeta tija kubwa kwa serikali kwani mwaka jana iliwez kuchangia asilimia 6 ya pato la serikali.

Alieleza kuwa hivi sasa Zanzibar ina wavuvi 40 elfu na wachuuzi 80 elfu na kueleza kuwa mafanikio yaliopatikana katika uzalishaji wa zao la mwani uko sawa na uzalishaji unaogfayika nchini Ufilipino.

Alieleza kuwa ndani ya miaka saba wavuvi wameongezeka kwa asilimia 87 na kueleza kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo ni kuwezsha kutumia uvuvi wa bahari kuu, kuwashajiisha wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar na kutumia vyombo vidogo vya uvuvi hadi leo.

Nae Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Amy Faust, alieleza kuwa Benki ya Dunia itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo na kueleza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni mafanikio ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuiwezesha Zanzibar katika uhufadhi wa rasilimali za bahari na kusisitiza kuwa benki hiyo itaendelea akuiunga mkono miradi mbali mbali iliyopo chini ya Wizara hiyo. Jengo hilo limejengwa na Kampuni ya DB Shapriya Co. Ltd ya Dar es Salaam kwa thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 1.6 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.