Dk. Sezibera aunga mkono masuala ya Jinsia kwa maendeleo endelevu

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera

Na Nicodemus Ikonko, EANA

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera amesisitiza umuhimu wa jamii kuheshimu masuala ya njinsia na kuonya kwamba kutofanya hivyo kutasababisha miradi mbalimbali kufa.

“Mipango mingi imeshindwa kutekelezeka kutokana na kutozingatia masuala ya jinsia mapema,” anasema Dk.Sezibera. Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Miundo Mbinu EAC, Phillip Wambugu wakati wa warsha ya wafayakazi wa EAC juu ya kuhusisha mashuala ya jinsia katika mipango na shughuli zao za kazi mapema wiki hii, alisisitiza kwamba wakati sasa umewadia wa kuangalia kwa undani kiasi cha manufaa yanayotokana na mchango wa jinsia katika miradi mikubwa mbalimbali.

“Jumuiya inaunga mkono masuala ya kuzingatia usawa wa jinsia na kuyaingiza katika mipango yote ya maendeleo na sheria,” alisema.

Mgeni rasmi katika tukio hilo ni Balozi Tegla Loroupe wa Kenya, mshindi mara mbili wa mbio ndefu za wanawake duniani.

Balozi Loroupe anafahamika sana katika kanda hii kwa juhudi zake za kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Pamoja na mambo mengine amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza mapambano ya kunyang’anyana mifugo kwa kutumia silaha, Kaskazini mwa Kenya, Kusini mwa Sudan, Kaskazini-Mashariki mwa Uganda na Ethiopia. Anasifika pia kwa kuleta amani katika maeneo hayo na kumpatia tuzo mbalimbali za kikanda na kimataifa.

Akihojiwa na Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) Balozi Loroupe alitoa wito kwa jamii za wafugaji kuwapeleka watoto wao shule kujifunza ujuzi mbalimbali kama njia mbadala ya kuendesha maisha yao badala ya kutegemea mifugo pekee.

Mwenyewe akiwa ametoka katika jamii hiyo, Balozi Loroupe alikumbusha kwamba wakati wa ukame mkali mifugo kama vile ng’ombe na mbuzi hufa karibu yote na kuziacha jamii hizo mikono mitupu na katika dhiki kubwa.

“Ujumbe wangu mwaka huu katika maazimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, kwanza siyo kwa wanawake bali kwa wanaume katika jamii za wafugaji wawasaidie watoto wao hususan wa kike kupata elimu ambayo itawawezesha kupata shughuli mbalimbali za kuendesha maisha yao,” alisisitiza.

Balozi huyo aliongeza kuwa “Wasichana wana haki ya kupata elimu kama wenzao wavulana. Jamii za wafugaji hazina budi kujifunza toka kwa jamii nyingine ambazo hupeleka shule watoto wao wa kike. Nao wafanye hivyo pia.”

Washa hiyo ndiyo iliyoanza shughuli mbalimbali za maazimisho ya wiki zima kati ya Machi 5 na 9, 2012 mkoani Arusha iliyopewa jina la ‘Wiki ya Jinsia’ iliyoandaliwa na Sekretariati ya EAC kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Taasisi ya Kanda ya Afrika Mashariki inayoshughulikia Haki za Binadamu na Wanawake (EASSI) na manispaa ya Arusha ikiwa ni sehemu ya harakati za maazimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani Machi 8.

Shughuli nyingine katika Wiki ya Jinsia ni pamoja na washa mbalimbali, maonyesho ya picha, vipeperushi, video na vitabu vinavyohusiana na masuala ya kupigania haki za wanawake na wasichana.