KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo, amezungumzia umuhimu wa taasisi za umma zilizo chini ya mradi wa Benki ya Dunia kuhakikisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), iliyofungwa inafanyakazi mara moja ili kuongeza tija na ufanisi katika kuhudumia wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua ufanisi wa matumizi ya TEHAMA katika hospitali ya rufaa ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Dkt. Sasabo amewataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha mifumo hiyo inakamilika na kuanza kazi mara moja.
“Hakikisheni ifikapo mwezi Septemba mawasiliano yenu na huduma zenu zilizounganishwa kwenye mifumo ya TEHAMA inafanyakazi ili kurahisisha utendaji na kuiongezea Serikali mapato”, amesema Dkt. Sasabo.
Dkt. Sasabo amemtaka Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya rufaa ya Dodoma Dkt. Samweli Seseja, kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa na mfumo maalum wa mawasiliano utakaowezesha kuboresha huduma katika hospitali hiyo na kumudu ongezeko la watu katika Manispaa ya Dodoma.
Akiwa wilayani Bahi, Katibu Mkuu huyo wa mawasiliano amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi Bi, Rachel Chuwa kuhakikisha mifumo ya Tehama iliyofungwa katika ofisi za halmashauri hiyo na katika shule za sekondari wilayani humo inafanyakazi mara moja ili kuendana na malengo ya serikali katika utoaji wa huduma bora, za kisasa na kwa wakati kwa wananchi wake na hivyo kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi zake zikiwemo ofisi, shule, hospitali na vituo vya polisi ili kuboresha huduma na kuwezesha uwazi katika ukusanyaji wa mapato na hivyo kuhamasisha wananchi kuchangia huduma kwa hiari.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.