Dk. Richard Sezibera afanya mabadiliko ya uongozi EAC

Dk. Julius Tangus Rotich, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa

Na Nicodemus Ikonko, EANA-Arusha

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Dk. Richard Sezibera amefanya mabadiliko ya majukumu ya kazi kwa manaibu wake watatu, ikiwa ni pamoja na kumhamisha Dk.Julius Tangus Rotich kutoka Kenya, kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa.

Dk. Rotich anachukua nafasi ya Beatrice Kiraso kutoka Uganda ambaye mkataba wake wa kazi umemalizika. Kabla ya kupewa nafasi hiyo mpya, Dk. Rotich alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Fedha na Utawala, nafasi ambayo sasa amepewa kuiongoza Jean-Claude Nsengiyumva kutoka Burundi.

Kwa mujibu wa taarifa ya ugawaji wa majukumu mapya kwa viongozi hao waandamizi wa EAC na nakala yake kuonekana na Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA), nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Nsengiyumva ya Naibu Katibu Mkuu, Uzalishaji na Sekta ya Jamii amepewa Jesca Eriyo, kutoka Uganda, ambaye ameteuliwa wiki iliyopita kuwa Naibu Katibu Mkuu.

Wakati huo huo, Dk. Enos Bukuku wa Tanzania anaendelea na wadhifa wake wa Naibu Katibu Mkuu, anayesimamia Mipango na Miundombinu.

Mkutano maalum wa 10 wa wakuu wa nchi wanachama wa EAC uliofanyika Mei 28, 2012 mjini Arusha, ulimwelekeza Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Sezibera kuwagawia majukumu manaibu wake wanne, kufuatia kuondoka kwa Kiraso na kuteuliwa kwa Naibu Katibu Mkuu mpya, Eriyo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maafisa hao wanaanza kazi zao mara moja.

Kiraso, ambaye kitaaluma ni mchumi, amepata majukumu mapya ya kuwa Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa nchi za Kusini mwa Afrika yenye makao yake makuu, Lusaka, Zambia.