Na Beatrice Mlyansi na Benjamin Sawe
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi ameitaka kamati mpya ya kubuni vazi la taifa kukamilisha mchakato wa kupata vazi hilo ndani siku 75 ili liweze kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi zaidi.
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kamati hiyo, Waziri Nchimbi amesema kazi ya kamati hiyo siyo kuanza mchakato upya bali ni kukamilisha mchakato wa kupata vazi la taifa la mwanaume na mwanamke ulioanza tangu mwaka 2004.
Amesema Wizara imefanya mambo kadha wa kadha katika kukamilisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kutembelea nchi kadhaa za Afrika ili kupata uzoefu wa namna walivyopata vazi la taifa. Amesema anaamini kwa kupitia mapendekezo ya awali ya kamati na taaluma yatasaidia mchakato huo ili kuwe na vazi la taifa.
“Mnayo kazi kubwa kwa sababu lazima tufike mwisho tuwape Watanzania kile ambacho wamekisubiri kwa muda mrefu, Watanzania wanatarajia ufanisi mkubwa kutoka kwa kamati hii.” Alisema Waziri Nchimbi. Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, Joseph Kusaga amesama watajitahidi kufanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha nchi inapata vazi la taifa kwa sababu ni kitu kizuri nchi kuwa na vazi lake.
Hivi Karibuni Waziri Nchimbi aliteua wajumbe wa kamati maalum inayoongozwa na Joseph Kusaga ambaye ni Mweneykiti ili kufankisha mchakato wa kupata vazi la taifa, wajumbe wengine walioteuliwa ni pamoja, Angela Ngowi Katibu, Joyce Mhavile, Mstafa Hassanali, Absalum Kibanda, Habibu Gunze, Makwaia Kuhenga na Ndesambuka Merinyo.
Wakati huo huo Waziri ametoa pole kwa Watanzania wote waliokumbwa na mafuriko yaliyosababisha kupoteza maisha kwa baadhi ya watu na mali kuharibiwa, pia amewapongeza wanahabari kwa kuhabarisha umma licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu.