Na Janeth Mushi, Arusha
WAZIRI wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema kitendo cha kuporomoka kwa maadili nchini kinatokana na
makabila mengi kupuuza na kutokuzingatia mila na desturi kama ilivyokuwa awali.
Waziri Nchimbi amesema hayo leo mjini hapa katika tarafa ya Enaboishu
wakati alipokuwa akizindua sherehe za jando kwa vijana wa kiume wa
rika la Ilkishiru wa jamii ya Kimasai zoezi ambalo linafanyika kwa
wakazi wa jamii hiyo waishio Ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema hivi sasa makabila mengi yamekuwa yakipuuza mila na desturi zao hali inayosababisha kuporomoka kwa maadili hususani kwa vijana.
Aidha ameongeza kuwa Wamaasai pekee ndiyo wanaoongoza kwa kufuata na kutunza mila na desturi zao ambapo amewataka kuhakikisha kuwa wanaendeleza utamaduni wao kwa vizazi vijavyo.
“Kwa niaba ya serikali nawapongeza wamasai kwa kudumisha mila na
desturi zao kwani kuan tatizo la makabila mengi hapa nchini kupuuza
mila zao jambo linalosababisha kuporomoka kwa maadili,” alisisitiza
Nchimbi.
Waziri huyo alisema kuwa iwapo Watanzania wataweza kuendeleza kudumisha mila na desturi zao itasaidia kuongezeka kwa maadili hasa kwa vijana ambao kwa hivi sasa maadili yao yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Nchimbi aliwataka vijana kuhakikisha kuwa wanazingatia suala la elimu
kwani mkombozi pekee kwa vijana pamoja na kuwataka wawe mstari wa
mbele kulinda rasilimali.
Awali akisoma risala kwa niaba ya wenzake, Moikan Mesheti amesema kuwa tatizo la kuporomoka kwa maadili ya vijana linatokana na utandawazi ulipo hivi sasa ambao umesababisha vijana wengi kukimbilia mijini kutafuta kazi.
Mesheti alisema kuwa mara ya mwisho tohara ilifanyika Oktoba,2004
ambapo kundi la vijana walio kwenye rika ya Korianga walitahiriwa na hivyo kuiomba Serikali kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za mila na desturi kupewa hati miliki ili waweze kuhifadhi mila na desturi zao.
“Tunaiomba Serikali kuhakikisha maeneo ya shughuli za mila
yaliyotengwa yanapewa hati miliki ili tuweze kuhifadhi mila na sesturi
zetu kwani kumekuwa na migogogro mingi ya maeneo ambayo husababisha tuenekane kama wakimbizi,” alisema.