Dk. Mwinyi Awataka Wataalam wa Afya Kuzuia Magonjwa

Dk. mwinyi aliyasema hayo leo (jana) wakati wa uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika jana jijini Dar es salaam ambapo alisema sekta ya afya na ustawi wa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko la milipuko ya magonjwa kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Frank John na Hassan Silayo- Maelezo

WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi amewataka wajumbe wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini, kufanya kazi kwa kujituma na ushirikiano ili kupambana na changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuzuia maambukizi ya magonjwa.

Dk. mwinyi aliyasema hayo leo (jana) wakati wa uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika jana jijini Dar es salaam ambapo alisema sekta ya afya na ustawi wa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko la milipuko ya magonjwa kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Alibainisha kuwa afya ya mazingira ni suala mtabuka ambalo linahitaji ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya afya ya mazingira ili kutoa matokeo yenye tija na ubora wa hali ya juu katika kupambana na magonjwa hayo.

Aliongeza kuwa serikali inatarajia kwamba kwa kutumia baraza hilo huduma ya afya ya jamii itatolewa kwa wananchi kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo, kuboresha maisha ya wananchi kwa kusimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi ya haki.

“Pia wataalam wa kada hii watajiendeleza na kufikia kiwango cha juu cha elimu tofauti na miaka iliyopita ampapo wengi waliridhika na kubaki katika eneo moja kwa muda mrefu na kusababisha kudumaa kwa taaluma,alisema Dk.Mwinyi.

Alisema kwa kufanya , hivyo upo uwezekano mkubwa wa kupunguza ongezeko la kasi ya magonjwa, vifo na madhara mengine katika jamii yatapungua ikiwa huduma ya afya ya jamii itaboreshwa.

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo , lililomaliza muda wake Bwana Fabian Magoma alisema linakabiliwa na changamoto za upungufu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za baraza na ukosefu wa mitaala hivyo linahitaji ushirikiano wa karibu na taasisi zinazoandaa mitaala ya elimu nchini.

Magoma alishauri baraza hilo, liangalie sheria zinazohusiana na afya ya mazingira, ili waweze kutambua taaluma hiyo. Huku akiongeza kuwa watu wanaoteuliwa kufanya kazi hiyo wawe ni wa kada hiyo.

Kwa upande wake mjumbe wa baraza jipya Haji Mdemu alishauri serikali kuzingatia mbinu za zamani za afya mazingira , kuzifufua ili kuimarisha afya mazingira na uwajibikaji wa maafisa afya.

Baraza hilo lilizinduliwa rasmi mwaka 2009 ikiwa ni matokeo ya sheria ya kusajili wataalam wa afya mazingira ya mwaka 2007 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiwa na majukumu ya kusajili, kudhibiti nidhamu kiutendaji katika kada ya afya ya mazingira pamoja na kumshauri waziri husika juu ya masuala yote yahusuyo afya ya mazingira nchini.